Stori: Imelda Mtema
SIKU chache zimekatika tangu kusambazwa kwa picha feki inayodaiwa ni ya mama wa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, Mariam Sepetu, wawili hao wako kwenye mkakati mzito wa kuwasomea kisomo cha Albadili wale wote waliohusika kwa namna yoyote ile kuitengeneza picha hiyo na kuitupia mitandaoni,
Wema Sepetu akiwa na mama yake, Mariam Sepetu.
Picha hiyo iliyosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwa
na kichwa cha mama Wema, lakini sehemu ya kuanzia shingoni kwenda chini
si yeye na mhusika alikuwa hana nguo, ilizua gumzo kwa wiki mbili sasa
huku watu wanaojiita Timu Dengue wakitajwa kuhusika.KINYWANI MWA CHANZO CHA HABARI
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mama Wema na mwanaye wameamua kusoma Albadili ili kuwaadabisha wale wote waliohusika na sakata hilo lenye kufedhehesha.
“Mama Wema na mwanaye walikasirishwa sana na watu waliotengeneza ile picha na kuitupia kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram.
“Wiki iliyopita baadhi ya wasamaria wema walikwenda nyumbani kwa mama Wema na kumtajia majina ya wahusika, lakini hawakuwa na ushahidi hivyo yeye na Wema wameamua kujiunga kiimani zaidi kwa kusoma Albadili.
“Wamesema kwanza kabla ya tukio hilo la Abdadili wametoa siku saba kwa yeyote anayejijua amehusika na picha zile za kutengeneza aende mwenyewe kwa mama Wema, nyumbani kwake, Sinza-Mori (Dar) ili kuomba msamaha.
“Kama zitapita siku saba na hakuna atakayejitokeza, Albadili itasomwa na mmoja baada ya mwingine watakufa. Tayari wameshawasiliana na mashehe ambao watasoma Albadili hiyo,” kilisema chanzo hicho.
WEMA AYEYUKA HEWANI
Baada ya kusikia kutoka kwa chanzo chetu cha uhakika, juzi Risasi Jumamosi lilimsaka Wema ili kumsikia anasemaje kuhusu kuwepo kwa madai hayo lakini muda mwingi wa maandalizi ya habari hii, simu yake haikuwa hewani!
MAMA WEMA SASA
Baada ya kumkosa Wema, Risasi Jumamosi lilimtafuta mama yake, naye kwa njia ya simu na alipopatikana aliombwa kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo.
KUHUSU ALBADILIAkizungumza kwa hasira huku sauti yake ikionesha dalili kwamba bado hayuko sawa, mama Wema alisema:
“Ni kweli, nimeshapanga kufanya hivyo, nitasoma Albadili. Haiwezekani watu wakae na kuamua kunichafua mimi, nimewakosea nini cha mno mpaka kufikia kufanya vile! Siwezi kukubali hata kidogo.”
KUHUSU MASHEHE
“Ni kweli pia, nimeshawasiliana na mashehe. Wao wako tayari wanachosubiri ni kupita kwa siku ambazo nimetoa. Kama hakuna atakayejitokeza kuomba radhi, kisomo cha Albadili kitasomwa, wataanza kupukutika mmoja baada ya mwingine kweli nasema.”
SIKU SABA ZINAANZA LINI?
“Jumamosi ijayo (leo) itakuwa siku ya kwanza. Kwa hiyo mpaka Ijumaa ya Julai 11 (mwaka huu), itakuwa siku ya mwisho.”
NENO LAKE KWA WAHUSIKA
“Nawaambia wale wote wanaojijua walihusika na ile picha ya uongo, ya kutumbukiza kichwa changu kwenye picha nyingine na wale waliohusika kuitupia kwenye mitandao, waje waniombe radhi kabla siku saba hazijaisha, sitanii jamani.”
UKWELI WAKE
“Mimi ni Muislamu safi, nasema sijawahi kupiga picha za namna hiyo katika maisha yangu tangu nizaliwe mpaka utu uzima wangu huu na wala sijawahi kufikiria.”
KUMBUKUMBU YA WEMA
Katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko, Toleo la Juni 25, mwaka huu, ukurasa wa mbele kulikuwa na habari yenye kichwa; Wema azimia!
Habari ile ilimhusu Wema kupoteza fahamu kufuatia kuiona picha hiyo kwenye mitandao akidai ililenga kumchafulia mama yake jina.
KILIO KWA TCRA
Kumekuwa na wimbi la watu kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii ambapo ukiacha watu maarufu kutengenezewa picha chafu, pia wanafunzi wa vyuo wamekuwa waathirika wakubwa.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliowahi kuzungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walitoa kilio chao kwa Wizara ya Sayansi na Teknolojia kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kudhibiti usambazwaji wa picha chafu mitandaoni.
VIA GPL
No comments:
Post a Comment