KUMEKUCHA!
Baada ya kuwepo kwa misuguano ya chini kwa chini kati ya viongozi na
wanachama wa kundi la waigizaji wa filamu la Bongo Movie Unity, sasa
siri imefichuka kuwa baadhi ya watu wanaotajwa kuwania kuteuliwa na
Chama cha Mapinduzi (CCM) ili wagombee urais mwakani, ndiyo wanaolibomoa
kundi hilo kutokana na fedha wanazodaiwa kuzitoa.
Baadhi ya waigizaji wenye ushawishi katika kundi hilo waliliambia
gazeti hili juzi kwamba, dhambi kubwa inayolitafuna kundi hilo ni kambi
za kisiasa zinazoratibiwa na makada wawili wanaoonekana kuwa na
ushawishi ndani ya CCM ambao wanatajwa kutaka kumrithi Rais Jakaya
Kikwete.
“Unajua hapa Bongo Muvi kuna watu wamejikita moja kwa moja katika
hizi kambi ambazo kuna waheshimiwa hawa wawili (majina tunayo) ndiyo
sababu kuu ya watu wengine kufikia kujiuzulu kwa hoja kuwa wanatumika
kwa manufaa ya mtu,” alisema mmoja wao aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Inadaiwa kuwa waheshimiwa hao wawili wamekuwa wakitoa fedha ili
kufadhili hafla mbalimbali zinazowahusu waigizaji hao kwa lengo la
kutaka kuwatumia muda rasmi wa kampeni utakapowadia.
“Hata hizi hafla zinabuniwa na kuratibiwa na wakubwa hao ambao hutoa
fedha za kutosha kwa ajili ya kuzifanikisha. Mfano, kujiuzulu kwa Katibu
wa Bongo Muvi, Mtitu (William) kulitokana na kuyeyuka kwa fungu
lililotoka kwa… (anataja jina).
“Sasa Mtitu akaona huu ubabaishaji, watu wengine wanufaike wao
watumike tu,” alisema mtoa habari huyo.Akizungumzia hitima ya kuwaombea
wasanii wa filamu waliotangulia mbele ya haki iliyofanyika hivi karibuni
katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambako Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi Taifa (CCM) Abdallah Bulembo alikuwa mgeni rasmi, mtoa
habari hii alisema kuna ‘fungu’ lilitoka.
Katibu wa Bongo Muvi aliyejiuzulu, Mtitu aliliambia gazeti hili kuwa
ni kweli amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa wanatumika kisiasa
kwa faida ya watu wengine.
“Nimechoka kutumiwa kisiasa bila ridhaa yangu, kisingizio Bongo Muvi,
kama kuna mtu au chama kinataka kututumia wasanii au kuitumia Bongo
Muvi basi kuwe na uwazi na siyo kumtumia mtu mmoja kwa manufaa yake
mwenyewe,” alisema.
Mwenyekiti wa Bongo Muvi, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ alipoulizwa
kuhusu ishu hiyo, alikiri kuzisikia siku nyingi, tokea alipoandaa
chakula cha usiku kwa wadau wake katika Hoteli ya Great Wall iliyopo
Masaki jijini Dar.
“Unajua si kila kitu ni siasa na yote haya yanasemwa kwa kuwa mimi
niko kambi ya huyo mheshimiwa. Kwa vile likitokea jambo lolote Bongo
Muvi mi huwa naenda kwake kuomba msaada.
“Halafu hakuna mwana Bongo Muvi asiyejua kuwa akaunti yetu ipo tupu,
sasa nikienda kuomba fedha naambiwa niko kambi yake, hilo halina ukweli
wowote,” alisema Steve anayehisiwa kuwa kambi hiyo.
Akikanusha madai ya kutafuna shilingi milioni 22 kati ya hizo, saba
zikiwa ni malipo waliyochukua kwa ushiriki wao katika tamasha moja na
zilizobaki zikiwa ni michango kutoka kwa matajiri mbalimbali, Steve
alisema:
“Ilitoka shilingi milioni saba kwa ajili ya tamasha, huyo Mtitu ni
mmoja wa watu waliokula zile fedha lakini hazungumzi chochote.
Kuhusu kupewa milioni kumi na tano na huyo mheshimiwa ili nifanye dua
pale Karimjee Hall si kweli, kuna watu kibao wametoa misaada yao na
uzuri zaidi hakuna aliyetoa fedha taslimu zaidi ya kusema mimi nitafanya
kitu fulani na wamefanya, mimi namsihi Mtitu awe mkweli tu katika hili
asituchonganishe.”
Makada wa CCM wanaotajwa kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha
bendera ya chama hicho 2015 ni Edward Ngoyai Lowassa, Frederick Tuluway
Sumaye, Steven Masatu Wassira, January Yusuf Makamba, Bernard Camillius
Membe, Wiliam Mganga Ngeleja, Samuel John Sitta na hivi karibuni
Mizengo Peter Pinda.
No comments:
Post a Comment