Stori: Mwandishi Wetu Dar na Jaed Kimaro, Bukombe TUKIO
la kutisha la kushambuliwa kwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe
mkoani Geita, ambapo askari wawili walipoteza maisha na silaha kadhaa
kuporwa, limeelezwa kuwa kwa kiwango cha asilimia mia moja, jambo hilo
ni ugaidi wa dhahiri.
Jumamosi iliyopita, majira ya saa sita
usiku, watu wasiojulikana, walikivamia kituo hicho kwa mabomu na silaha
zingine nzito zinazosadikika kuwa ni za kivita, wakafanya mauaji na
kujeruhi watu wengine kadhaa kabla ya kupora bunduki na silaha
zilizohifadhiwa kituoni hapo.
“Huu siyo ujambazi wa kawaida uliozoeleka,
ni kweli kuna wakati matukio yanatokea kuwa ya kutisha sana, lakini aina
hii ya mashambulio siyo kawaida, tena kituo cha polisi? Hawa watu ni
dhahiri walihitaji kupata silaha tu, sasa sijui zinakwenda kutumika wapi
na tuna shaka kama hawa si Watanzania,” alisema Zebareta Shayo, mkazi
wa Sinza, jijini Dar es Salaam.
Waziri Salum, mwanasheria na wakili wa
kujitegemea alisema tukio hilo ni vizuri kama lingeifanya serikali
kutazama upya mipaka yetu kwani kuna kila dalili kuna baadhi ya wageni
wanaingia kirahisi na kufanya unyama huo bila kujulikana.
Askari waliopoteza maisha katika shambulio
hilo wametajwa kuwa ni Uria Mwandiga mwenye namba WP 7106 na Dustan
Kimati mwenye namba G 615 PC. Majeruhi ni David Ngupama Mwalugelwa (44)
namba E 5831 APL na Mohamed Hassan Kilomo (25) namba H 627 PC.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa baada ya Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini, (IGP) Ernest Mangu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) Isaya
Mngulu kuwasili tangu juzi mkoani hapa, askari zaidi kutoka Mikoa ya
Tabora, Shinganya na Mwanza wanaendelea kuwasili.Msako mkali unaendeshwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kuweza kuwabaini wahalifu hao huku Kamanda wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo akiwataka wananchi kutoa taarifa mara moja watakapotilia shaka nyendo za mtu yeyote ili kurahisisha zoezi hilo alilodai lazima lifanikiwe.
Juni 10, mwaka huu, tukio kama hilo likihusisha majambazi waliokisiwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo na kujeruhi mgambo mwingine kisha kupora bunduki tano na risasi 60.
No comments:
Post a Comment