Utafiti
ambao umefanyika unaonesha kuwa, asilimia kubwa wapo kwenye uhusiano na
watu ambao siyo waliopangiwa na Mungu kuwa nao.Kutokana na hilo ndiyo
maana utakubaliana na mimi kwamba, usaliti umekuwa ukishamiri, watu
wamekuwa wakiachana kila siku na wengine kuendelea kuishi pamoja lakini
si kwa amani.
Hii
ni kwa sababu wameingia kwenye penzi na watu ambao si sahihi. Kutokana
na mazingira hayo, haiwezi kuwa kitu cha ajabu mume wa mtu kutokea
kumpenda sana mke wa mtu au kinyume chake.
Pia huwezi kuonekana mwendawazimu kwa kumpenda mtu ambaye tayari ana
mpenzi wake. Hii ni kwa sababu inawezekana una mapenzi ya kweli zaidi
kwake kuliko huyo aliye naye. Hata hivyo, hakuna kitu kibaya kama
kuanzisha uhusiano na mtu ambaye tayari ana mpenzi wake au ameshaingia
kwenye ndoa. Utakuwa unatafuta matatizo kama utamtongoza mke wa mtu au
utaonesha kumzimikia mume wa mtu na kujikuta ukishawishika kutaka
kumpasulia ukweli.
Madhara yake ni makubwa kwani kuingilia uhusiano wa watu kunaweza
kuyagharimu maisha yako. Wapo ambao wameuawa kwa kuwapenda wake za watu.
Yawezekana si kwa u-kiwembe wao bali mapenzi ya kweli waliyonayo lakini
ukweli unabaki kwamba, unayempenda tayari ana mtu wake, wewe huna jinsi
tena. Itakubidi ubaki ukiumia moyoni huku wakati mwingine ukiomba hata
waachane ili wewe uweze kuchukua nafasi. Hiyo inatokea sana huko
mtaani.
Sasa basi, ni yapi ambayo unatakiwa kuyafanya pale ambapo umetokea
kumpenda mtu ambaye tayari ana mtu wake? Kwanza kabisa, hakikisha
unafanya kila uwezalo ajue kile kilichomo moyoni mwako. Tumia mbinu
yoyote kumpata na kumpasulia ukweli. Utamueleza jinsi unavyompenda na
namna anavyokukosesha amani lakini mwisho wa siku mweleze kwamba
humaanishi aachane na huyo aliyenaye bali kokote atakakoenda ajue yupo
mtu f’lani, sehemu f’lani anampenda.
Ukifanikiwa kufanya hivyo, angalau unaweza kubaki na amani. Kunaweza
kuwa na ugumu kumpata kutokana na mazingira hasa ukichukulia kwamba
kunatakiwa kuwe na usiri mkubwa sana kwenye kufikisha ujumbe huo. Pili,
hakikisha unaonana naye mara kwa mara. Hiyo angalau itakupunguzia
machungu hasa kama na yeye atakuwa na chembechembe za kukupenda.
Ukibahatika kuonana naye akiwa peke yake, msalimie kwa kumchangamkia
huku ukionesha kufarijika kukutana na mtu ambaye ana nafasi kwenye moyo
wako. Tatu, weka kumbukumbu kwa kumnunulia zawadi ndogo au kubwa ambayo
itamfanya kila anapoiangalia akukumbuke. Isiwe zawadi ambayo inaweza
kumletea matatizo kwenye uhusiano wake. Kwa mfano, kama ni mwanafunzi
unaweza kumnunulia kalamu au leso, vitu ambavyo hata mpenzi wake hawezi
kumshitukia. Kama ni mtu mnayefanya kazi au mnasoma pamoja, siku
mojamoja mkikutana hotelini, mlipie bili ya chakula au kinywaji.
Fanya
hivyo bila mtu mwingine kujua. Unajua kwa nini hii inatajwa kuwa moja
ya njia inayoweza kukufanya ukawa na amani? Ni kwa sababu endapo
ataipokea zawadi ama ofa yako, utabaki na furaha hata kama hajakukubalia
wewe uwe mpenzi wake.
Kumbuka unafanya hayo yote si kwa ajili ya kumtega wala kumshawishi
achepuke au amuache mpenzi aliyenaye awe na wewe, unafanya hayo kuonesha
upendo wako kwake lakini pia kutafuta amani ya moyo. Tahadhari kubwa
unayotakiwa kuichukua ni kuhakikisha humshawishi kufanya naye mapenzi
wala kumuonesha upendo wako katika mazingira ambayo yeye asingependa.
Kwa mfano, yawezekana kutokana na unavyomzimikia ukajikuta unatamani
kumpigia simu na kuongea naye au kumtumia hata sms nzuri.
Usithubutu kabisa kufanya hivyo kwani unaweza kumfanya akuogope na
asikuchangamkie akihisi utamharibua uhisiano wake. Pia epuka kuonesha
upendo wako kwake akiwa na marafiki zake. Ukifanya hivyo inawezekana
mmoja wa marafiki zake anajuana na mpenzi wa huyo unayempenda kisha
akazifikisha taarifa ikawa tatizo. Mawasiliano yako na yeye ikiwezekana
iwe mnapoonana tu akiwa hayuko na mpenzi wake.
Hii ni kwa sababu unaweza kumtumia sms kumbe simu anayo mpenzi wake
au ukampigia simu akapokea mpenzi wake na kusababisha matatizo kwa
mwenzako. Mwisho naomba niseme kwamba, unapotokea kumpenda mtu ambaye
yuko kwenye uhusiano, hata kama na yeye anakupenda, chukulia kwamba
huwezi kumpata tena.
Tafuta mwingine ambaye utamuonesha mapenzi yako na hakikisha
unapambana na hisia zako za kumpenda mpenzi wa mwenzako kwani
ukiziendekeza, zitakutesa sana. Nihitimishe kwa kukuambia wewe msomaji
wangu kwamba, kumpenda mtu mwingine licha ya kwamba uko kwenye uhusiano
wala si dhambi, ni hali ya kawaida ya kibinadamu inayowakumba wengi.
Kikubwa ni kuwa makini katika kila unachokifanya ili uendelee kuishi
maisha ya furaha na amani lakini pia huwezi jua, yawezekana siku moja
Mungu akatimiza aliyopanga na huyo unayempenda akaingia mikononi mwako.
Kumbuka subira inahitajika katika kila jambo!
No comments:
Post a Comment