Aliyekuwa
Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtemvu katika pozi na mshindi wa pili,
Lillian Kamazima (kulia) pamoja na mshindi wa tatu, Jihhan Dimachk.
Sitti amelivua taji hilo baada ya kuiandikia barua kamati ya Miss Tanzania, November 5 mwaka huu, kuhusiana na uamuzi wake huo.
Mrembo huyo alikuwa akikabiliwa na shutuma za kudanganya umri wake, jambo ambalo lilililazimu Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA kutokana na agizo la wizara husika kufuatilia ukweli wake.
“Baada ya kutwaa taji la urembo la Miss Tanzania kumezuka shutuma mbalimbali dhidi yangu. Wameniwekea maneno mengi sana mdomoni kwamba nimesema wakati sio,” amesema kwenye barua hiyo.
Sitti Abbas Mtemvu
“Shutuma hizo zimeandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari, blogs na mitandao ya kijamii, kiasi ambacho naweza hata kuhatarisha maisha yangu. Sasa kwa hiari yangu tena bila kushawishiwa na mtu na kwa kulinda heshima yangu na familia yangu natamka rasmi kuvua taji la urembo la Miss Tanzania 2014,” ameongeza.
“Napenda niwashukuru wale wote waliokuwa wakinipa sapoti tangu mwanzo nilipoingia katika mashindano haya katika ngazi ya taifa, na warembo wote wa Chang’ombe, Temeke pamoja na wote tuliokuwa nao katika fainali za Taifa. Pia napenda kutuma shukrani za dhati kwa waandaji wote wa kituo cha Chang’ombe, Temeke na wajumbe wa Kamati ya Miss Tanzania kwa mafunzo mbalimbali niliyopata. Nawashukuru pia waandishi wote kwa mchango wenu, pamoja na wizara ya habari, utamaduni na michezo na Baraza la Sanaa kwa busara zenu.”
“Leo nalivuta taji rasmi nililopewa na binadamu lakini alilonipa mwenyezi Mungu bado analo. Mwisho naomba radhi Watanzania wote kwa uamuzi huo niliochukua.”
Nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa mshindi wa pili, Lilian Kamanzima.
No comments:
Post a Comment