Johannesburg, Afrika Kusini. Familia ya nahodha wa timu ya taifa
ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’, Senzo Meyiwa imemzuia mpenzi wa
mwanasoka huyo na mama wa mtoto wake, Kelly Khumalo, kuhudhuria mazishi
yake mjini Durban, kwa mujibu wa New Age.
“Mazishi haya yapo wazi kwa kila mtu kuhudhuria na kutoa heshima zake za mwisho kwa Senzo, lakini yule msichana (Kelly Khumalo) haruhusiwi. Asifikirie kabisa kuhusu hilo,” alinukuliwa baba wa Meyiwa, Samuel.
Ofisa Upelelezi wa Gauteng, Meja Jeneali Norman Taioe aliwaambia waandishi wa habari mjini Johannesburg jana kwamba Meyiwa alipigwa risasi kifuani alipokuwa amekwenda kumtembelea mpenzi wake, ambaye ni mwanamuziki na msanii, Kelly
Khumalo, katika mji wa Vosloorus, Ekurhuleni Jumapili usiku.
Wanaume wawili waliingia katika nyumba hiyo wakati kipa huyo mwenye miaka 27 wa timu ya taifa na klabu ya Orlando Pirates akijiandaa kutoka na mpenzi wake. Mmoja kati ya wauaji hao alikuwa nje.
“Senzo na rafiki yake walikuwa wanatoka wakati watu wawili wakiingia ndani ya nyumba hiyo. Mmoja wa watu hao alimdhibiti mmoja wa marafiki wa Senzo,” Taioe alisema Jumatatu.
Risasi moja ilipigwa ndani ya nyumba na mbili nyingine zilipigwa ovyo nje. Watu hao walifanya tukio hilo na kuiba simu.
Zawadi nono ya Rand 250,000 imetangazwa kutolewa kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika.
Polisi ilitoa michoro ya sura za watu wawili
wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo wakiwa na rasta kichwani na mmoja ana
jino la dhahabu. Meyiwa anatarajiwa kuzikwa mjini Durban kesho.
Wakati huo huo; kunatarajiwa kuwa na maziko ya nyota watatu wa Afrika Kusini Jumamosi, Mbulaeni Mulaudzi, Senzo Meyiwa na Phindile Mwelase, ambao wataagwa kwenye ukumbi wa Standard Bank mjini Johannesburg.
Nahodha wa Bafana Bafana na Orlando Pirates, Meyiwa aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Vosloorus Jumapili, wakati mshindi wa dunia wa zamani wa mbio za mita 800, Mulaudzi alipoteza maisha katika ajali ya barabarani, Ijumaa iliyopita.
Bondia wa kike, Mwelase alifariki dunia baada ya kushindwa kuamka tangu alipoanguka na kupoteza fahamu wiki mbili zilizopita.
Awali, familia ya Meyiwa iliombwa na klabu ya Orlando Pirates kumzika kipa huyo Jumapili kutokana na wingi wa maziko ya watu maarufu siku hiyo.
Lakini, baba yake, Samwel Meyiwa alikataa ombi hilo na kusisitiza kuwa mtoto wake atazikwa Jumamosi kama walivyopanga awali.
No comments:
Post a Comment