Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo ameongoza Sherehe za
Siku ya Mazingira Duniani na Siku ya Wangari Maathai kwa kuteketeza kwa
moto tani 15 ya pembe za ndovu zilizokuwa zikisafirishwa kimagendo.
Sherehe hiyo iliyofanyika katika Mbuga ya Wanyama ya Nairobi
ilihudhuriwa na wageni 1,000 akiwemo
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika, mawaziri, maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi
wa nchi mbali mbali duniani.
Aidha leo pia ni Siku ya Mazingira Afrika
ambayo huadhimishwa ili kufahamisha umma umuhimu wa kulinda mazingira ya
bara Afrika. Kuanzia mwaka 2012 siku hiyo huadhimishwa pamoja na Siku
ya Wangari Maathai ili kumuenzi mlinda mazingira hiyo wa Kenya aliyepata
Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na jitihada zake za kulinda mazingira.
Katika ujumbe wake kwa mnasaba wa siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa Ban Ki-moon amesema biashara haramu ya wanyamapori na bidhaa
zitokanazo na viumbe hivyo ikiwemo ndovu, magogo na kifaru, imekuwa
ikiibuka na mbinu mpya kila uchao na hata kuzidi ile ya usafirishaji
haramu wa binadamu na madawa ya kulevya.
Amesema kushamiri huko
kunapigiwa chepuo na rushwa na uongozi dhaifu akiongeza kuwa kuna
ushahidi thabiti wa kuhusika kwa mitandao ya kihalifu iliyopangwa na
vikundi vilivyojihami.
No comments:
Post a Comment