MWANASIASA mashuhuri Visiwani Zanzibar,
Balozi Amina Salum Ally, ameandika historia ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa
kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, huku akiainisha vipaumbele
vyake 11.
Wakati Balozi Amina akifungua milango ya uthubutu kwa wanawake, mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aitwaye Makongoro Nyerere naye ametinga mkoani Dodoma alasiri ya leo na kukabidhiwa fomu katika Makao Makuu ya CCM.
Ikumbukwe kwamba, Balozi Amina ambaye
amewahi kushika nyadhifa kadhaa za uwaziri visiwani ikiwemo wizara nyeti
ya fedha, pia amewahi kujitokeza kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa CCM
kuwania urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuleta mchuano mkali.
Akizungumza na waandishi baada ya
kukabidhiwa fomu yake, Balozi Amina amesema kipaumbele chake cha kwanza
ni kuwa na chombo maalum cha kusimamia masuala ya uchumi na maendeleo
ambacho kitakuwa na jukumu la kutoa ushauri wa haraka kuhusu maeneo na
aina ya uwekezaji unaohitajika.
Amesema chombo hicho kitasaidia kuondosha
ucheleweshwaji wa maamuzi ya uwekezaji, kuondoa mikataba mibovu na ya
hasara isiyo na tija kwa taifa.
“Kipaumbele kitawekwa kwa sekta
zitakazochangia haraka moja kwa moja kupunguza umasikini, kwa mfano,
kilimo na viwanda, serikali itabuni njia bora za kukuza uhusiano kati ya
uwekezaji na ukuaji wa viwanda na kilimo kuanzia wakulima na
wajasiriamali wadogo wadogo hadi wakulima na viwanda vikubwa,”amesema.
Amezitaja njia kuu za usafirishaji kuwa
itakuwa ni njia pekee ya kukuza uchumi ambazo ni pamoja na reli,
barabara, na usafiri wa baharini sambamba na maziwa huku akiahidi
kufufuliwa au kujengwa upya ili ziweze kuchangia haraka kukua kwa
uchumi.
Amefafanua kuwa Tanzania ina idadi kubwa
ya wanawake ambapo takwimu zinaonesha idadi ya wanawake wote ni
takriban milioni 25 zaidi ya nusu ya watanzania wote ambao wanahitaji
kutambuliwa na kupewa fursa sawa kwa kushirikishwa kikamilifu katika
upangaji wa matumizi ya rasilimali za kitaifa.
Kwa imani ya Balozi Amina, hilo
linawezekana ikiwa wanawake watashirikishwa au kuwezeshwa kushiriki
katika mipango yote ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hasa
katika maeneo ya kutoa maamuzi yaayogusa jamii.
Amesema serikali yake itapigania kuondoa
kasoro za mfumo dume ambao bado unachangia kudumaza huduma za msingi kwa
wanawake huku akitolea mfano pamoja na elimu ili kuweze kupatikana
maendeleo ya haraka.
“Mimi ninaamini, kwa wingi wao, mkakati
wa kumuendeleza na kuwainua kimaendeleo wanawake wa kitanzania utakuwa
ni njia nzuri pia ya kuwainua watanzania kutoka katika ufukara wa kipato
na kielimu pia,”amesema.
Kipaumbele chake cha pili ni utoaji wa
huduma za jamii kwa usawa kwa wote ikiwa takribani miaka 50 nchi
imegubikwa na tatizo la huduma duni kwa jamii huku akitolea mfano wa
afya na kinga za mama na mwana ili kupunguza vifo.
Pato la Taifa
Kuhusu mgawo bora wa pato la taifa,
amesema kwa takribani miaka kumi iliyopita pato la nchi limekuwa
likikua kwa kiwango kinachoridhisha huku ukuaji wake haujaambatana na
kuwaletea maisha bora watanzania walio wengi.
“Kwangu tofauti hiyo kubwa ya kipato
katika jamii ni hatari kwa mustakbali wa umoja wa kitaifa na
amani na utulivu wa kuletea nchi yetu maendeleo. KUa kuna kila sababu ya
kimsingi inayohitaji utekelezaji wa haraka wa kuwepo mgawo bora wa pato
la taifa,” amesema.
Elimu
Balozi Amina amesema kuporomoka kwa ubora
wa elimu katika ngazi zote ni changamoto kubwa katika nchi ikiwa ni
pamoja na wahitimu kukosa uwezo au elimu ya kutosha kupata au kujiajiri
wenyewe ili waweze kujikimu kimaisha.
Ameahidi kuhakikisha elimu wanayopata
vijana inawawezesha katika kukabili kikamilifu ushindani katika soko la
ajira ndani na nje ya nchi.
Utawala wa Sheria
Balozi Amina ameahidi kuweka mazingira
bora ya kisheria katika kuwezesha uwekezaji katika uzalishaji mali na
kuendesha biashara na miradi mikubwa nchini.
Amesema ili kukuza haraka ukuaji uchumi
na kushinda vita dhidi ya umaskini ni vyema kukubali kuwa mchango wa
sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa nchi unahitaji kusimamiwa
vyema kwa wawekezaji wa nje kuwekewa mazingira mazuri.
Ukusanyaji kodi
Ameainisha kuwa takwimu za kitaifa
zinaonyesha bayana kushuka kwa ukusanyaji wa kodi nchini mwaka hadi
mwaka tangu mwishoni mwa miaka ya 1990s.
Kwa mujibu wa Balozi Amina, mapungufu
ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukusanyaji huo yamekuwa yakileta
adha nyingi kwa serikali na hata kwa watanzania huku akitolea mfano
kushuku au kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii.
Rushwa
Amesema rushwa, ufisadi, uwajibikaji
usioridhisha na ukosefu wa maadili ni mambo ya msingi ya kushughulikia
kwa taifa linalofuata sera ya uwazi na utawala bora na maadili mema.
Kwamba, Tanzania imeingia doa kutokana na
kugubikwa na vitendo vya ufisadi, rushwa na mapungufu makubwa ya
ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji serikalini takriban katika ngazi
zote.
“Mimi naamini, serikali ni lazima iwe
inawahudumia wananchi wake wote kwa kusimamia upatikanaji wa huduma bila
ya ufisadi na vitendo vya rushwa kwa kufanya hivyo, wananchi watakuwa
na imani na serikali yao,”amesema.
Muungano
Balozi Amina ametamba kuwa, akipewa
ridhaa ataendeleza mchakato wa kupata Katiba mpya ambao ulisimamiwa na
serikali ya awamu ya nne na kwamba yeye ni muumini wa uhakika wa
utawala.
Amesema kuwa Katiba bora itavusha taifa kwenda katika hali ya juu ya maendeleo na amani na utulivu.
Lugha
Pia amegusia lugha ya Taifa akisema
Kiswahili kwa ajili ya mawasiliano ya aina mbalimbali ni moja ya tunu na
nguzo zinazoliweka taifa kuwa kwenye umoja upendo na mshikamano ambao
ndio ulioupatia amani na usalama.
Ameseme kutokana na hali hiyo, Kiswahili
kinatakiwa kiendelezwe kudumishwa kama lugha ya Taifa na kwamba kutokana
na kuongezeka kwa mashirikiano ya kibiashara, kisiasa na kitamaduni
kati ya Tanzania na nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara,
inabidi kitumike na kisimamiwe katika ufundishaji nyenzo ya kuwapatia
vijana ajira.
Makongoro Nyerere achukua fomu
Mwanasiasa huyo, ambaye ameingia kwenye
kinyang’anyiro kwa tambo za kutaka kuwabana aliowaita “vibaka” ndani ya
CCM, ametinga kuchukua fomu akiongozana na Mzee Chifupa na kisha
kuelezea ratiba ya kukusanya wadhamini akianzia Singida na Tabora.
Amesema kuwa, atazunguka na usafiri wa
gari ambalo alikopa kwenye ubunge wa Afrika Mashariki na kwamba yeye
hana uwezo wa kifedha kama wengine huku akitamba kuwa hata waliofika
Butiama kumsikiliza walijigharamia.
Kwa mujibu wa Makongoro, serikali ya CCM
ina watu maarufu sana ambao pia ni maarufu kwa kutoa na kupokea rushwa
na kusababisha kushusha heshima ya chama pamoja na kukigawa katika
makundi ya ukabila na udini.
Kuhusu ilani ya chama, amesema kuna wengi
waliosema akiingia madarakani ataweka uchumi wa kati, wakulima wataacha
jembe la mkono, jambo alidai huo ni uongo kwa vile wagombea sio
wanaotengeneza ilani ya chama.
Ratiba ya kesho
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM
Makao Makuu, kesho saa 4:00 hadi 5:30 asubuhi, atakayekuwa wa kwanza
kuchukua fomu ni Amos Siyatemi. Kati ya saa 5:30 hadi 7:00, atachukua
Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye.
Baadaye kuanzia saa 7:00 hadi 8:30
mchana, itakuwa zamu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano,
Dk.Mohamed Gharib Bilali, akifuatiwa na Balozi Ally Karume kati ya 8:30
hadi 10:00 alasiri.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya
Richmond, Edward Lowassa zamu yake itakuwa kuanzia saa 10:30 hadi 11:30
alasiri huku Dk. John Magufuli akifunga dimba kwa siku hiyo kati ya
11:30 hadi 12:30 jioni.
No comments:
Post a Comment