Uongozi wa mabingwa wa Kombe la
Kagame, Yanga ya jijini Dar es Salaam umesema kuwa zoezi la kumpata
mrithi wa kocha aliyetangulia, Mserbia Kostadin Papic linakwenda
taratibu kutokana na dau kubwa la mishahara ambayo makocha
wanaowapendekeza wamekuwa wakitaja, imefahamika.
Hata hivyo, uongozi huo umekataa kutaja majina ya makocha wanne waliosalia katika kinyang'anyiro hicho ila wamethibitisha kwamba kwamba wanatoka nje ya nchi.
Hata hivyo, uongozi huo umekataa kutaja majina ya makocha wanne waliosalia katika kinyang'anyiro hicho ila wamethibitisha kwamba kwamba wanatoka nje ya nchi.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja
wa wajumbe wa Kamati ya Usajili, Abdallah Binkleb, alisema kuwa
wanajipanga kufanya maamuzi sahihi na hawataki kukurupuka tena katika
kuajiri kocha mpya ambaye atakiongoza kikosi chao.
Binkleb alisema kuwa hawataki
kufanya maamuzi watakayojutia baadaye na vile vile wanataka kupata kocha
ambaye ataipa Yanga mafanikio katika msimu ujao wa ligi.
"Kabla ya kuamua tunaangalia mambo
mengi, kubwa likiwa ni gharama zake na uzoefu alionao... safari hii
hatutaki kutimua tena kocha ndani ya muda mfupi," alisema Binkleb.
Aliongeza kuwa wanataka kupata
kocha mwenye wasifu mzuri na ambaye atakainua kiwango cha wachezaji wao
na kufanya vizuri kwenye msimu ujao.
"Tunataka kuwa na kocha ambaye
ataipa Yanga mafanikio na tuwe na uvumilivu kwa kuangalia kazi na si
kumtimua kama ilivyofanyika kwa makocha waliopita," Binkleb aliongeza.
Alisema kwamba hivi sasa bado
wanamuamini Fred Minziro kuwa atakisimamia vyema kikosi chao licha ya
mashindano ya Kombe la Kagame kukaribia.
Aliongeza kuwa ubora wa wachezaji
waliowasajili unawafanya wajiamini kwamba msimu ujao, Yanga itakuwa na
matokeo mazuri kwa sababu kila aliyejiunga na timu hiyo ana kiu ya
mafanikio.
Yanga imeshasajili nyota kadhaa
wakiwemo Ally Mustafa 'Barthez' na Kelvin Yondani kutoka Simba, Frank
Domayo (JKT Ruvu), Juma Abdul, Saidi Bahanuzi (Mtibwa Sugar), Ladslaus
Mbogo (Toto African) na Simon Msuva wa Moro United.
Yanga itacheza mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 14 hadi 29 hapa nchini.
Mbali na Yanga, timu nyingine
kutoka Tanzania Bara zitakazoshiriki michuano hiyo inayoandaliwa na
Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ni Simba na Azam
za Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment