UJIO wa waimbaji wa kwaya ya Kanisa la Waadiventista Wasabato ya
Rwanda ‘Ambassador of Christ’ maarufu kama ‘Kwetu Pazuri’ hapa nchini,
umezua gumzo baada ya waimbaji hao kupewa ulinzi wa hali ya juu ulioleta
kadhia kwa wapenzi na mashabiki wa kwaya hiyo.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, katika mkutano unaoendela
kwenye viwanja vya Biafra Kinondoni, waumini hao walidai kuwa ulindwaji
wa waimbaji hao na mabaunsa, unaleta karaha kwao na ni kinyume na imani
ya dini hiyo inayowataka wote kuwa sawa.

Wakitolea mifano, mmoja wa waumini hao Daniel Jonas alisema kuwa
Jumamosi iliyopita walijikuta wakikosa radha ya mikutano hiyo, hasa pale
walinzi hao walipowasukuma hovyo waumini waliokuwa karibu na wanakwaya
hao wakati wakipita.
“Nchi yetu ina amani, sidhani kama kuna mtu wa kutaka kuwadhuru waimbaji hao ambao ni kipenzi cha wengi hapa nchini,” alisema.
Kwaya hiyo iliyojipatia umaarufu, hasa baada ya kuja nchini mara ya
kwanza na kufanya maonesho makubwa na yenye mafanikio, wamekuwa wakija
nchini mara kwa mara, lakini utaratibu wao wa kutumia mabaunsa umeanza
kutumika awamu hii, ambapo inawakera washiriki wa dhehebu hilo na
mashabiki wao, ambao kimsingi ndiyo wenyeji wa wanakwaya hao.
Habari kutoka ndani ya uongozi wa kanisa hilo, zimeeleza kuwa, vijana
hao hawakuwekwa na kanisa bali ni kampuni moja inayoshughulika
kusambaza kazi zao.
Uongozi huo pia ulisema kuwa lengo la kuweka walinzi hao ni kutaka
kupunguza kero na msongamano kutoka kwa wapenzi wa kwaya hiyo.Habari na Happiness Mnale wa Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment