WADAU wa elimu zaidi ya 100 kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki wanatarajiwa kushiriki maonesho ya elimu
yanayotarajiwa kufanyika Julai 10 hadi 13 mwaka huu kwenye Viwanja vya
Nanenane jijini hapa.
Katika maonesho hayo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk.
Richard Sezibera anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi
huo.
Mratibu wa maonesho hayo, Neema Kaaya kutoka Kampuni ya East Africa
Education Tanzania Ltd aliiambia Tanzania Daima juzi kuwa tayari
maandalizi yote yamekamilika.
Alisema kuwa maonesho hayo yatawakutanisha wadau wa elimu
wanaojishughulisha na uuzaji wa vifaa vya elimu, vikiwemo vitabu, zana
za kufundishia, nguo za wanafunzi, samani za shule pamoja na wamiliki
wa shule na vyuo mbalimbali kuanzia shule za awali, msingi, sekondari
mpaka vyuo vikuu kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Kaaya aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi wakati wa maonesho hayo
ili waweze kupata taarifa muhimu juu ya masuala yanayohusiana na
elimu.
Alisema maonesho hayo yanaweza kuwasaidia wazazi kufahamu taarifa
mbalimbali kuhusu mfumo wa elimu unaofuatwa kwenye shule mbalimbali,
ambazo zitakuwa kwenye maonesho hayo, hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi
ni wapi wawapeleke watoto wao kupata elimu.
Kaaya alisema kuwa kwenye maonesho hayo wamiliki wa shule na vyuo
mbalimbali watapata fursa ya kueleza kwa kina kuhusiana na mambo
mbalimbali ya kitaaluma wanayotoa kwenye shule zao, ikiwemo kuweka wazi
juu ya sifa za kitaaluma za walimu, wakufunzi na maprofesa walio nao
kwenye shule na vyuo vyao. Habari na Grace Macha, Arusha wa Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment