MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama ‘Sugu’
(CHADEMA), amempiga kijembe Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Suleiman Kova, akimtaka arudi
studio atengeneze vizuri filamu ya utekwaji wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Sugu alisema filamu iliyopo hivi sasa haileweki kwenye jamii, kwa kuwa
tukio hilo limegubikwa na utata, hasa baada ya Mchungaji Kiongozi wa
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kuibuka na kudai kuwa
mtuhumiwa aliyekamatwa na jeshi hilo ni mwendawazimu.
Kijembe hicho alikitoa juzi jioni bungeni alipokuwa akichangia hotuba
ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2012/2013.
Alibainisha kuwa licha ya serikali na Bunge kufunga mjadala juu ya
kutekwa kwa Dk. Ulimboka, kwa madai kwamba suala hilo liko mahakamani,
ukweli utabaki kuwa filamu hiyo haikuchezwa vizuri.
“Jambo hili lina utata sana, hivi sasa wanajaribu kuliingiza katika
mambo ya kidini, Kamanda Kova filamu yako haieleweki….katengeneze
nyingine,” alisema.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimzuia Sugu kuendelea
kugusia jambo hilo, kwa kuwa tayari Bunge lilikwisha kubaliana
kutolijadili suala hilo kwa sababu lipo mahakamani.
Wiki iliyopita Kamanda Kova alitangaza kukamatwa raia wa Kenya, Joshua
Mulundi (21), akihusishwa na utekaji huo, na kwamba mtuhumiwa huyo ni
muumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe.
Kova alidai raia huyo mwenye kitambulisho cha utaifa namba 29166938
kilichotolewa Oktoba 11, 2010 katika Wilaya ya Nyeri nchini Kenya, pia
anamiliki hati ya dharura ya kusafiria yenye namba 0123431 iliyotolewa
Juni 14 mwaka huu huko Namanga, Kenya.
Alisema mtuhumiwa huyo na wenzake 12 wako kwenye kikundi kijulikanacho
kama Gun Star, chenye makao yake Iwiru, Wilaya ya Thika nchini Kenya na
kwamba kinaongozwa na mtu mmoja ajulikanaye kama Silencer, akisaidiwa
na Paft.
Alisema pia mtuhumiwa huyo alidai kuwa wamekuwa wakijihusisha na
matumizi ya silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya uhalifu
nchini Kenya.
Alisema baada ya utekaji huo, Juni 29 mwaka huu raia huyo alikwenda
katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe kwa nia ya kutaka kuonana
na kiongozi wa kanisa hilo, Mchungaji Gwajima, lakini hakufanikiwa
badala yake alionana na msaidizi wake ajulikanaye kama Joseph Marwa
Kiriba.
Siku mbili baada ya polisi kutoa taarifa hizo, Mchungaji Gwajima
alikana mtu huyo kwenda kutubu kanisani kwake, bali alikamatwa nje ya
viwanja vya kanisa hilo na walinzi.
Alisema mtu huyo alionekana kurukwa na akili, kwani alikuwa akipiga
kelele, jambo lililowafanya walinzi kumchukua na kumpeleka polisi.
Katika hatua nyingine, Sugu aliitaka serikali kuunda tume huru
kuchunguza vurugu zilizotokea Novemba 11 mwaka jana mkoani Mbeya, ambazo
ziliwahusisha polisi na wafanyabiashara ndogondogo.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment