WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, jana
aliibua madudu mengine ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo
ilinunua misumari kwa pauni 50,000 badala ya spea.
Muhongo aliongeza kuwa baadhi ya wabunge wakiwamo wale wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wanafanya biashara na
TANESCO, ambapo kampuni ya mbunge mmoja ililiuzia shirika hilo mataili
mabovu.
Waziri huyo aliibua madudu hayo alipokuwa akijibu hoja za wabunge
waliochangia hotuba ya bajeti yake kwa mwaka 2012/2013 ambapo alisema
serikali haitasita kuiingilia TANESCO pindi inapobaini mambo hayaendi
sawa.
Alisema kuna taarifa za siri kutoka kwa wabunge watatu kuwa biashara
ya nguzo imekuwa ikifanyiwa mchezo mchafu kwa kuchukuliwa mkoani Iringa
na kupelekwa Afrika Kusini na kisha kurejeshwa hapa nchini na kuuzwa
bei kubwa.
Aliongeza kuwa TANESCO ina madudu mengi na wamemuagiza Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi ndani ya
shirika hilo.
“Waheshimiwa wabunge naomba tumwachie CAG afanye uchunguzi kama
tulivyomuagiza na habari za kamati teule tuachane nazo na kufunga
mjadala huu hata kwenye vyombo vya habari tuchape kazi,” alisema.
Waziri Muhongo alianza kujenga hoja zake akinukuu kauli mbili za
mwanafalsafa na mwandishi wa habari mkongwe kuwa; “Ukweli ni tochi au
kurunzi ndani, hivyo kadiri unavyoitingisha ndivyo inavyowaka” na
“Ukitaka kujua mafanikio ya kiongozi yeyote aliyefanikiwa ni kutazama
yale ya wenzake waliyoyaacha.”
Katika hilo aliweka bayana kuwa mtu yeyote anayeitetea TANESCO au wale
wote wanaowaumiza wananchi ni mpuuzi, kwa vile shirika hilo limekuwa
likifanya kazi tangu mwaka 1930 lakini kwa miaka yote hiyo wameshindwa
kusambaza umeme kwa asilimia 20.
“Anayedhani TANESCO haitaingiliwa anajidanganya tu. Hii ni ajabu,
maana hatuwezi kuchukua vyanzo vya mapato ya serikali kwenye bia kila
mwaka badala ya TANESCO,” alisema.
Kuhusu kuunda tume kwa mambo ambayo yanakuwa yametokea ndani ya wizara
yake, Waziri Muhongo alisema utaratibu mpya anaoupendekeza sasa ni ule
wa watendaji pamoja na yeye kwenda eneo husika na kukutana na wananchi
kusikiliza (public hearing).
Tuhuma za Mhando
Kuhusu tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,
William Mhando, alisema kuwa amesimamishwa kupisha uchunguzi wa
matumizi mabaya ya fedha na madaraka.
Alizitaja tuhuma zinazomkabili Mhando kuwa ni pamoja na kukiuka sheria
ya maadili ya umma kwa kuingia mkataba wa kutoa mkopo wa sh milioni
884.5 kwa kampuni ambayo ana masilahi nayo, kwani mkewe Eva ndiye
mkurugenzi, na watoto wao wawili (Veronica na Fredy).
Kuhusu hofu ya kuwapo kwa mgawo wa umeme, Waziri Muhongo alisema kuwa
ilikuzwa tu na mafaisadi kwa kupitia mawakala wao lakini akabainisha
kuwa shirika linao uwezo wa kutosha kuzalisha umeme.
Ni katika mlolongo wa hujuma hizo, waziri alibainisha kuwa madai ya
kwamba wizara ilikiuka kanuni ya manunuzi ya umma kwa kuipa mkataba
Kampuni ya PUMA Energy wa kusambaza mafuta kwa Kampuni ya IPTL kwamba si
za kweli.
“TANESCO haikuwa na fedha, vile vile mafuta, lakini ilitaka iweke
masharti kwa kampuni ya kuisambazia mafuta. Siku wanapoweka mgawo
hawakunipa taaarifa wala wasaidizi wangu. Watu hao hao waliokata umeme
kwa kusingizia kukosa mafuta nilikwenda ofisini kwao kesho yake
nikitokea Dodoma, lakini nikakuta bado hawajanunua mafuta,” alisema.
Prof. Muhongo alifafanua kuwa fedha walizowapatia TANESCO
hazijaingilia utaratibu kwani hawakuingia huko kuwashawishi waipe zabuni
PUMA Energy.
Alisema kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na serikali kwa asilimia 50,
hivyo kununua mafuta kwake wanapata unafuu na gawiwo la hisa, lakini pia
walibaini ujanja kwamba hata kampuni iliyokuwa ipewe zabuni ya kuuzia
mafuta TANESCO kwa sh 1,800 kwa lita, nayo inayanunua kwa PUMA Energy
kwa bei ndogo ya sh 1,460.
“Tumepata barua ambayo tungeitumia kama nondo ya kutuokoa humu ndani
kama wabunge msingeshutukia mchezo uliokuwa ukifanyika dhidi yetu. Hii
ndiyo ingetuokoa maana inaonesha kuwa kwa vile IPTL ipo chini ya
mufilisi, mkataba unabainisha wazi kuwa Wizara ya Nishati na Madini
ndiyo yenye mamlaka ya kuinunulia TANESCO mafuta,” alisema.
Kuhusu Bodi ya TANESCO nayo kuvunjwa kutokana na kukosa uhalali wa
kimaadili, waziri alisema wanaelekea huko na hivyo kubainisha kuwa hata
wajumbe wake kuanzia sasa watapaswa kuomba kazi na kusailiwa kwa
kulingana na sifa zao.
Katika hatua nyingine, Waziri Muhongo amaeanza kutekeleza maagizo ya
kupunguza matumizi ya serikali kwa vitendo ambapo amepiga marufuku
watendaji wake kutumia magari ya anasa, maarufu kama mashangingi na
kwamba viongozi wakuu watatumia magari yasiyozidi CC 3000, ambayo
watakopeshwa.
Alisema kwa kufanya hivyo, wizara yake itaokoa kiasa cha sh bilioni
1.4 kila mwaka, fedha ambazo zitaelekezwa kwenye matumizi mengine ya
maendeleo.
Pia alikubaliana na hoja ya msemaji wa kambi ya upinzani, John Mnyika,
ya kuitaka serikali kuweka akiba ya dhahabu, akisema jambo hilo ni la
msingi na kama kuna mchumi atalikataa itabidi wamtilie shaka.
“Kwa mfano, unaweza kuona wenzetu wa mataifa makubwa walivyojizatiti
katika hilo, mathalani Marekani inaongoza kwa kuweka akiba ya tani
8,133.5, ikifuatiwa na Ujerumani 3,396.3, IMF tani 2,811.1, Italia
2,451.8, Ufaransa 2,435.1, China 1,054 wakati Afrika Kusini inashika
nafasi ya 29 ikiwa na tani 125,” alisema.
Wezi wa umeme waanikwa
Waziri Muhongo pia aliwataja wezi sugu wa umeme ambao wamekuwa
wakitumia nishati hiyo kwa kutumia luku za wizi ambazo hazijasajiliwa na
TANESCO ambapo katika orodha hiyo imo shule maarufu ya kimataifa ya St.
Mary’s inayomilikiwa na mmoja wa wabunge wa Viti Maalumu, Mchungaji
Gertrude Rwakatare.
Alisema kuwa shule hiyo imetumia umeme wa sh milioni 10.5 huku wezi
wengine wa Dar es Salaam wakitajwa kuwa ni Access Benki ya Tabata sh
milioni 13.8, Shree Shalim sh milioni 8.1 na Hoteli ya Akubu Paradise
mali ya Philip Ngunda iliyoko eneo la Kariakoo.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment