SPIKA AVUNJA KAMATI YA NISHATI, WAZIRI AELEZA WALIVYOITAFUNA TANESCO
WAKATI
wabunge wakitoa tuhuma nzito dhidi ya wenzao wanaodaiwa kujihusisha na
ufisadi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imebainishwa kuwa
wabunge wenye tabia hiyo ni watano, watatu kutoka chama tawala CCM na
wawili upinzani.
Habari zilizopatikana jana
mjini Dodoma zimeeleza kuwa baadhi ya wabunge hao wanatoka katika Kamati
ya Bunge ya Nishati na Madini, huku wengine wakitoka Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Mashirika ya Umma.
Kwa mujibu wa
taarifa hizo, wabunge hao wamedaiwa kuwa wamekuwa wakitumia nafasi zao
za ubunge na ujumbe wa kamati kufanya biashara na Tanesco na kutetea
mafisadi ndani ya shirika hilo la umma.
Gazeti hili limefanikiwa kupata majina ya wabunge hao, ambayo leo hatutayataja kwa sababu za kitaaluma.
Baadhi
ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni juzi na jana walisema kuwa,
wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini hawapendi kuwataja kwa kuwa
siyo wakati mwafaka.
Moto wa kutaka kutajwa kwa
majina ya wabunge hao ulikolezwa jana na Mbunge Vita Kawawa wa
Namtumbo(CCM) aliyeomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hili lijadiliwe
na Bunge na kupendekeza kuwa, Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa
zivunjwe.
“Waheshimiwa wabunge wamejadili
suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa kifungu cha 55 (3)f
mbunge au waziri anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe. Sasa
naomba kutoa hoja ya kujadili suala hilo," Kawawa alisema.
Aliliomba
pia Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini
na kamati nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa. Hoja hiyo iliungwa
mkono na wabunge.
Baada ya hoja hiyo kuungwa
mkono Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kukubali hoja hiyo ya
Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.
Spika
Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge
kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea
rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.
"Ninakubali
kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zingine ambazo zitatajwa kwenye
tuhuma hizo. Nalipeleka pia suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili
na Madaraka ya Bunge, halafu kama ni kutajwa (wabunge hao), basi
tutapata mwongozo wa kamati hiyo." alisema Spika Makinda na kuongeza:
"Nasema
kwa dhati kabisa, kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge hili.
Wabunge mkae vizuri. Kama kuna baadhi yetu wanaenda huku na huku
kujitafutia masilahi binafsi, tutawezaje kuisimamia Serikali?"
Mbunge Zedi
Baada
ya Spika kutangaza kuvunja Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa
Kamati ya Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema kuwa ameshtushwa na
uamuzi huo na anasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya
Bunge.
"Nimeshtushwa sana na uamuzi huo, lakini tusubiri Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge," alisema Zedi.
Waziri Muhongo
Akihitimisha
hoja ya wizara yake bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alisema kuwa baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye
vikao vya uamuzi vya Tanesco kama wajumbe, wamekuwa wakilihujumu
shirika hilo kwa njia mbalimbali ikiwamo kufanya nalo biashara.
"Shirika
liliwahi kulipa Pauni za Uingereza 50,000 kwa ajili ya kununua vipuri,
lakini kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari,” alisema Profesa
Muhongo na kuongeza;
“Hata katika nguzo za
umeme kuna biashara inaendelea. Tunajua kuwa nguzo hizo zinazalishwa
Iringa na kupelekwa Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo kwamba
zimetoka Afrika Kusini."
Waziri Muhongo
alisema kuwa mbali na ufisadi huo, baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa
Kamati ya Nishati na Madini wamewahi kuliuzia shirika hilo matairi ya
magari kwa bei kubwa, bidhaa ambayo hata hivyo alisema haina ubora
unaokubalika.
"Baadhi ya wabunge wanafanya
biashara na Tanesco; niseme tu kuwa, hii siyo sahihi. Lakini niombe
kwamba mjadala huu tuufunge kwa sababu, tayari tumekabidhi suala hilo
kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)" alisema Waziri
Muhongo.
Waziri Muhongo pia alizungumzia jinsi
baadhi ya watu na kampuni zinavyoiibia Tanesco kupitia mita za Luku
ambapo aliwataja watu hao kuwa ni pamoja na Shule za St. Mary's
zinazodaiwa Sh10.5 milioni, Access Bank, Tawi la Tabata Matumbi Sh13.8
milioni na Hoteli ya Akudo Paradaise ya Kariakoo inayodaiwa Sh25.5
milioni.
Alisema kuwa baada ya kubainika kwa
wadaiwa hao hutumia umeme kinyume na utaratibu,wahusika wote
walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi baada ya kufanyika kwa
uchunguzi.
“Baada ya kufanya uchunguzi na
kubaini kuwapo kwa watu wanaotumia umeme bila kulipia na kuisababishia
Tanesco hasara, tumeamua kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafikisha polisi,”
alisema Profesa Muhongo na kuongeza:
“Inaonyesha
wazi kwamba wizi wa umeme wa Luku umekuwa ukifanyika mara kwa mara na
kwamba baada ya kuwakamata hawa, uchunguzi utaendelea na wengine
watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.”
Jenista Mhagama
Katibu
wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kuwa, amepokea kwa
masikitiko taarifa hizo za wabunge wa CCM kuingia katika tuhuma hizo,
lakini akasema namna nzuri ya kushughulikia tatizo hilo ni vyombo vya
dola kufanya uchunguzi makini ili kujiridhisha na kisha hatua za
kisheria kufuatwa.
"Ni taarifa mbaya kwa kweli,
lakini mimi niiombe Serikali itusaidie kufanya uchunguzi ili ukweli
ubainike na hatua zichukuliwe," alisema Mhagama.
Mbunge Silinde
Naye
Katibu wa Wabunge wa Chadema, David Silinde alisema: "Kwa kuwa
tumesikia, kama kambi tutafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo. Tutakaa
kikao cha kuamua nini cha kufanya. Pia tutatoa tamko juu ya mwenendo
mzima wa hizi tuhuma na Bunge kwa ujumla.”
Zitto
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma ambayo imeunganishwa kwenye
tuhuma hizo, Zitto Kabwe, alisema tuhuma hizo anazisikia, lakini
anaziona kama siasa za majitaka kwa sababu zinarushwa bila ushahidi
wowote.
"Hakuna hata mbunge mmoja aliyesimama
kusema nani amehongwa nini. Mimi binafsi sijahongwa na mtu yeyote wala
mimi sijamtetea mtu isipokuwa natetea taratibu kufuatwa," alisema.
Zitto
alibainisha kuwa anaamini tuhuma hizo zimetokana na hasira za yeye
kupinga posho za wabunge na sasa wameona hilo ndilo eneo la kumkomoa.
"Kwa
kuwa ‘my conscious is clear’, (dhamira yangu safi) sina mashaka,
uzushi, uongo na siasa za majitaka hizi zitaumbuliwa na ukweli. Hata
hivyo, kwa kuwa tuhuma hizo zinasemwa juu juu tu, tutataka vyombo vya
dola vichunguze na ikithibitika hatua zichukuliwe," alisema na kuongeza:
"Kwangu
mimi naona hizi ni siasa za urais na hasira za posho. Wenye kutaka
urais wa vyama vyote na wapambe wao, wameungana kunichafulia heshima
yangu. Wabunge wenye njaa ya posho, wameungana kunikomoa. Ukweli una
tabia ya kutopenda kupuuzwa. Mwalimu Nyerere (Julius) alisema katika
andiko lake la 'Tujisahihishe'.”
Mbunge huyo wa
Kigoma Kaskazini(Chadema) alishauri pia Spika wa Bunge kutumia Kamati
ya Maadili kuchunguza tuhuma hizo kwa kuwa hazipaswi kuachwa zikapita
hivihivi.
John Cheyo
Mwenyekiti wa
Kamati ya Hesabu za Serikali, John Cheyo alisema anasikitika kuona Bunge
ambalo kimsingi ni kitovu cha uadilifu limeanza kuvamiwa na mafisadi.
"Very
unfortunate, (bahati mbaya sana) Bunge ambalo ni kilele cha uadilifu,
nyumba ya waheshimiwa, ambako kunatarajiwa high level of intergrity
(uadilifu wa hali ya juu), kuanza kutumika kama perpets (vibaraka) wa
mafisadi," alisema.
Cheyo aliongeza: "Ninalaani
sana kitendo hicho, lakini niwaambie viongozi wapya wa Wizara ya
Nishati na Madini kuwa, waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na nguvu yao
ni wabunge wengi wema, ambao watawaunga mkono. Wasikate tama," alisema.
Mjadala ya wabunge
Mbunge
wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda aliliomba Bunge kufanya
uchunguzi ili kuwabaini wabunge wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema baadhi ya wabunge wanatumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuiyumbisha Serikali.
“Namwomba
Spika na timu yake yote ikaona kuna haja ya kufanya uchunguzi kwa
wabunge ili kuweza kuwabaini wanaotumia nafasi zao vibaya kwa
kujihusisha na vitendo vya rushwa ilikuiyumbisha Serikali ,” alisema
Shibuda
Mbuge Kangi
Naye
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora alitaka Waziri wa Nishati na Madini
awataje wabunge aliowatuhumu ili kuonyesha usawa hasa baada ya kuwataja
kwa majina watuhumiwa wengine katika ufisadi wa Tanesco na wale
wanaoliibia umeme shirika hilo la umma.
"Tunaomba
waziri asema kwa nini asiwataje hao wengine wakati tayari ametutajia
kina Freddy na Veronica William Mhando na taasisi za St Mary? " alihoji.
Hoja hiyo ya Lugora ilitupwa na Spika wa Bunge Anne Makinda aliyesema kuwa jambo hilo lina taratibu zake.
Kamata
Vicky
Kimata (Viti Maalumu) nusura amwage machozi bungeni juzi jioni,
alipozungumza kwa uchungu kupinga hatua ya wabunge hao kujihusisha na
ufisadi, huku akieleza kuwa nchi imefika pabaya.
'Watanzania tumefikia hapo! Watu wanatengeneza mgawo wa umeme ili kujipatia hela, Jamani...jamani.. Hammwogopi hata Mungu!"
Said Mussa Zuberi alipendekeza itungwe sheria ya kuwanyonga mafisadi na wahujumu uchumi kwa kuwa matendo hayo pia ni uuaji.
"Katika
taifa letu tuna wadudu sijui tuwaite mchwa ambao wanaharibu
yaliyotengenezwa kwa maslahi yao. Nawashauri wananchi kwa kuwa sasa tuko
kwenye suala la Katiba, wasisahau kupitisha sheria ili watu wahujumu
uchumi tuwaue, tena kwa risasi.
No comments:
Post a Comment