Mwanafunzi
wa darasa la pili jijini Dar es Salaam amefanyiwa unyama wa kutisha na
mama yake mzazi kwa kuchanjwa na viwembe mwili mzima na kumsababishia
kushindwa kwenda shuleni kutokana na kupata maumivu makali.
NIPASHE Jumapili ilifanikiwa kufika katika
eneo la tukio huko Mbezi Temboni mtaa wa Gape na kuzungumza na
mwanafunzi huyo wa kiume mwenye umri wa miaka nane aliyesema kuwa mama
yake, Jane Maparuwe alimchanja na viwembe maeneo ya mgongoni na kwenye
paja juzi majira ya saa 5:00 usiku.
Akisimulia mkasa huo mtoto huyo alisema
kuwa alikula maharage baada ya kusikia njaa kwa muda mrefu na mama yake
aliporudi nyumbani na kuanza kuulizia yaliyopo maharage hayo, alimwambia
kuwa amekula ndipo alipomkamata na kuanza kumpiga na kumchanja na
kiwembe.
Alisema mbali na kuchanjwa pia alipigwa kwa kutumia mkanda huku akimkwaruza na kucha zake usoni na kumwachia alama.
Alisema kutokana na kipigigo hicho
alishindwe kwenda shuleni kwa kuwa alikuwa na maumivu makali ya mguu na
mgongo. Alisema mpaka sasa hapati huduma ya hospitali na kwamba mama
yake mdogo alinunua plasta na kumbandika katika kidonda cha mguuni.
Alisema katika kipindi chote amekuwa akiishi na mama yake na kwamba baba yake Nassor Hassan anaishi eneo la Mwananyamala.
Hata hivyo, mtoto huyo amekuwa akiishi
maisha ya tabu kwani mama yake huwa anaondoka na kwenda katika biashara
zake za kuchoma mihogo na kurudi usiku, huku mtoto huyo akisubiri huruma
ya majirani kumpa chakula. "Huwa ninashinda peke yangu mama anakwenda
katika biashara zake anarudi saa 3 usiku huwa nakula kwa majirani wakati
mwingine ananipa hela ya kununua juisi na skonzi," alisema.
NIPASHE Jumapili ilifanikiwa kuzungumza na
Mjumbe wa shina namba nane katika mtaa huo wa Gape, Pendaeli Kahaya,
ambaye alisema majira ya saa 6 :15 mchana akiwa katika shughuli zake
alipigiwa simu na majirani zake na kumjulisha tukio la mtoto kuchanjwa
na viwembe na kisha kufungiwa ndani.
Alisema fundi ujenzi mmoja ambaye huwa
anafanya ujenzi katika nyumba hiyo alitaka maji ya kunywa, alipoingia
ndani alishangaa kukuta damu zikiwa zimetapakaa na ndipo alipomuuliza
mpangaji mwenzake.
"Fundi huyo alijibiwa kuwa kuna mtu
alikuwa anakula mali yake alipomuuliza ni kwanini amchanje chanje na
kumfungia ndani mpangaji huyo alimjibu hawezi kuelewa ndipo fundi huyo
alipokwenda kumuangalia," alisema Kahaya.
Kahaya alisema kabla ya mama huyo
kumchanja kwa viwembe alichukua kisu na kumtaka kumchinja mtoto huyo
lakini mdogo wake aliingilia kati na kumueleza kuwa ataondoka kama
atathubutu kufanya kitendo hicho.
Alisema mdogo wake aliondoka na ndipo mama
wa mtoto huyo alipoamua kumuagiza mtoto wa jirani kwenda kununua
viwembe na kuamua kumchanja na kumfungia ndani kwa siku mzima.
Hata hivyo, alisema wakati mtoto huyo
akifanyiwa tukio hilo jirani yake aliamka na kumuuliza ni kwanini
anampiga mtoto huyo kwa muda mrefu lakini mama huyo alimtukana jirani
huyo na kumtaka afuatilie mambo yake na sio ya kwake.
Alisema tukio hilo lilimsikitisha na
kuamua kwenda kumjulisha diwani wa kata ya Msigani, Rogati Mbowe, na
kumwambia aende kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali za mtaa.
Aidha, alisema aliwasiliana na uongozi wa
serikali za mtaa ambao ulichukua hatua juu ya suala hilo na askari
walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kumkamata mama huyo.
Alisema wameshangazwa kuona mtoto huyo
mpaka sasa hajapelekwa hospitali na pia mama huyo ameshaachiwa na
polisi jambo ambalo limewashtua wakazi wa eneo hilo.
"Sijaelewa sababu ambayo polisi imepelekea
mama huyo kuachiliwa tunataka kuona sheria inachukua mkondo wake maana
nilijiuliza maswali mengi hivi ni mtoto wake aliyemzaa kwa kumbebea
mimba ya miezi tisa na kuamua kumchanja na viwembe," alisema. NIPASHE
ilifanikiwa kuzungumza na diwani Mbowe ambapo alisema kuwa ni kweli
tukio hilo limetokea na kwamba kesho atalifuatilia kwa ukaribu kwani
alikuwa amepata majukumu mengine.
NIPASHE ilimtafuta mama mzazi wa mtoto
huyo katika sehemu yake ya biashara eneo la Kimara Temboni lakini
wafanyabishara wenzake walidai kuwa alikuwa ameshaondoka katika biashara
zake na kuelekea nyumbani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo hakuweza kupatikana.
Hata hivyo, habari za ndani ambazo limelifikia gazeti hilo ni kwamba polisi wameagizwa kumkamata mama huyo ambaye aliachiwa.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment