TUKIO la msanii Naseeb Abdul ‘Diamond’ kutinga Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam na njiwa wanne, kwenye Tamasha la Matumaini
lililofanyika hivi karibuni, limezua mitazamo tofauti kwa mashabiki,
huku wengine wakiingiza imani za kishirikina.
Tanzania Daima, lilishuhudia baadhi ya mashabiki wakirumbana katika
gari la abiria, lililokuwa likitoka Ubungo kuelekea Mlandizi, ambako
ubishi ulianza mara baada ya dereva wa gari hilo kuweka wimbo wa
Diamond, unaokwenda kwa jina la ‘Mawazo’ unaotamba vilivyo hivi sasa
hapa nchini.
Huku wimbo huo ukiendelea, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la
James Charles, alisema, anampenda sana Diamond, lakini kitendo
alichokifanya kinaonesha ishara ya ushirikina, huku akimtaka kuwaweka
wazi mashabiki juu ya maana ya kushuka uwanjani na njiwa.“Bwana wewe
Diamond ni mkali na mimi binafsi namkubali, ila kitendo cha kuingia na
njiwa, binafsi kimenifanya nibaki mdomo wazi, ni vema angetupa tafsiri
ya njiwa wale, anaanza kufanya nimuone wa ajabu na mwenye kuamini
ushirikina,” alisema Charles.
Charles alipozidi kujitwika msimamo huo, dada mmoja aliyejitambulisha
kwa jina la Aisha Rashid, alisema kuwa, naye anamuunga mkono James kwa
kuwa kitendo hicho, ingawaje hakuwepo uwanjani, lakini kwa sasa kimekuwa
gumzo kwa wadau mbalimbali hapa nchini.
“Tunakubali kuwa, Diamond ni mkali, lakini kama anatafuta umaarufu kwa
kufanya uchawi sio ishu, mimi simsapoti hata kidogo kwa hilo, bora
angefanya kama wenzake ambao walipanda bila ya kuonyesha vitu hivyo,
iwapo kweli ni mchawi, basi ajue hayo yanamwisho wake,” alisema Aisha.
Akizungumzia tukio hilo, Diamond alisema, kuingia kwake Uwanja wa
Taifa na njiwa wanne, ilikuwa ni sehemu ya burudani tu na ubunifu kwa
ajili ya kuwafurahisha wadau na mashabiki waliokuja katika tamasha hilo
kwa lengo la kuburudika.
“Kufanya kwangu hivyo, ni sehemu tu ya utashi na mbwembwe za
kiburudani, si imani za kishirikina, kama ambavyo mashabiki na wapenzi
wamekuwa wakifikiria,” alisema Diamond ambaye alipambana na mkali kutoka
Uganda, Jose Chameleon.
Via Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment