NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla,
amesema kuwa studio ya muziki iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa
ajili ya kuwanufaisha wasanii wa ndani bado haijazaa matunda na mpango
wa kuikabidhi serikalini unafanyika.
Akizungumza bungeni mjini hapa juzi, alisema pamoja na nia njema ya
kutaka kuwasaidia wasanii, lakini wajanja wachache wamekuwa
wakijinufaisha wao wenyewe kwa kutafuna fedha za studio hiyo.
Naibu waziri huyo aliongeza kuwa, wasimamizi hao wa studio
wamethubutu kutafuna sh milioni 9.6 zilizotolewa na Rais Kikwete kwa
ajili ya pango la studio hiyo na bila aibu wamekuwa wakiomba fedha
nyingine kwa ajili hiyo.
Hata hivyo, Makalla alisema kuwa kutokana na studio hiyo kutokuwa na
tija, serikali kwa sasa inafanya utaratibu wa kuirudisha serikalini na
iwe chini ya usimamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Aidha, alitangaza kiama kwa baadhi ya wajanja, ambao wanafanya ujanja
wa kuiba kazi za wasanii kwa kudurufu kazi zao kwa lengo la
kujinufaisha wao wenyewe badala ya wasanii husika.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni bora wale wote wenye mitambo ya
kudurufu kazi za wasanii, ambao wana tabia ya kuwaibia, wazirejeshe
wenyewe la sivyo watachukuliwa hatua kali.
Akiendelea kuelezea hoja za kambi rasmi ya upinzani bungeni, Makalla
alisema kuwa juhudi za Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu
kama Mr. II au Sugu, (CHADEMA), ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara
hiyo, alisema ni msaada mkubwa kwa serikali na wasanii kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment