KUTEKWA, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha
Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa Gazeti
la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni
ya simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye mtandao mpana
nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na
wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri
ya simu za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.
Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za simu zinazodaiwa
kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka, Afisa
Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.
Rais Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya
televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa vyombo
vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa
na kumtupa daktari huyo porini.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali
yake haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “…serikali imteke ili
iweje?”
Hivi karibuni serikali ililifungia Gazeti la MwanaHalisi baada ya
kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa
Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na
kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na
matibabu kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa ni ya
uchochezi, MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na
watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea
kuchunguzwa na kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai (DCI).
Vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi waliokumbwa na
sekeseke hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi ni wafanyakazi wa
kitengo cha IT ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri ya
mawasilino kati ya Dk. Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya
wake.
Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kampuni ya Tigo, aliliambia gazeti hili
kuwa mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi,
wafanyakazi wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya udanganyifu kwenye
huduma za Tigo Pesa na kujipatia fedha.
“Kweli watu wengi wamefukuzwa wakituhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la
MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa wakishirikiana na mawakala wa Tigo
Pesa kuiibia kampuni.
“Kwa mfano mfanyakazi alikuwa anakubaliana na wakala kumwingizia
kiasi kama cha sh milioni moja, lakini anaweza kuingiza hadi sh milioni
1.5 na kati ya hizo sh 500,000 ni mali yake,” alisema mfanyakazi huyo.
Akizungumzia na Tanzania Daima Jumatano, Mhariri Mkuu wa Gazeti la
MwanaHalisi, Jabir Idrissa alishangazwa na taarifa za Tigo kuwafukuza
wafanyakazi wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa na gazeti lake.
“Chanzo chetu cha habari hakikutoka kwa wafanyakazi wa Tigo. Kama
wamefukuzwa kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea bure. Kama Tigo ndio
waliotupa taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilitoka
wapi?” alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa bure.
Ofisa Uhusiano wa Tigo, Edward Shila, alipohojiwa kuzungumzia tukio
hilo, hakukubali wala kukataa madai hayo na kumtaka mwandishi kumtumia
maswali kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea majibu kiofisi.
“Kama una maswali naomba uniandikie kupitia e-mail yangu ambayo
nakutumia sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli yoyote isiyokuwa ya
kiofisi,” alisema.
Naye Omary Matulla ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa wa kitengo
cha kumbukumbu katika kampuni hiyo, alikanusha kuwapo kwa taarifa za
kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Alisema kuwa kila mfanyakazi ana mipaka ya kufanya kazi katika
kampuni hiyo, na pia ni wajibu wa kila mtumishi kutunza siri kubwa.
“MwanaHalisi ana mbinu zake za kupata habari wala haiwezekani kupata
habari kupitia kampuni yetu na hata hivyo jambo hilo si rahisi hata
kidogo kutokea,” alikanusha Omary.
Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26, kusukumizwa kwenye gari,
kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno na
hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar
es Salaam.
Tangu kutokea kwa tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati wa kutetea haki za
binadamu, wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo
iliyohusika.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman
Kova, hivi karibuni alitangaza kumfikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai
kukiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa, polisi wamekamata mtu
aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kumteka na kumtesa
Dk. Ulimboka.
Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima alikana
kauli ya Kova juu ya mtuhumiwa huyo, akisema hajakwenda kutubu kwao.
No comments:
Post a Comment