KAMATI ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, imesema majeshi ya Tanzania
yapo tayari kiakili na kivifaa ikibidi kuingia vitani kutokana na mzozo
wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Edward Lowassa alipozungumza na waandishi na habari na kusisitiza
Tanzania inaomba isifike katika hatua hiyo, lakini ikibidi wanajeshi
wetu wapo imara kutetea mipaka ya nchi hadi tone lao la mwisho la damu.
“Jeshi letu lipo tayari, na tumeridhika na utayari wao na
‘commitment’ yao. Sisi ni moja ya jeshi lililojiandaa vizuri sana na
miongoni mwa majeshi mazuri duniani. Tunajivunia vijana wa Tanzania
waliopo kwenye jeshi letu. Tupo imara kiakili, vifaa vya kisasa,”
alisema.
Alisema kamati hiyo inaunga mkono kauli ya serikali iliyotolewa juzi
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe,
kwani ni sahihi inayoelezea msimamo wa Tanzania kuhusu jambo hilo.
Alisema kuwa wanategemea jambo hilo litamalizika kidiplomasia ndani
kwa ndani ama ikibidi kuomba msaada wa watu wengine kusuluhisha kwa kuwa
Tanzania na Malawi ni marafiki na ndugu.
“Watu waliopo mipakani ni ndugu, tusingependa kufika mahali
kutokuelewana mpaka kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kwa
faida ya Watanzania tumepewa maelezo ya jeshi letu, tumeridhika kwamba
ikibidi jeshi letu limejipanga vizuri sana.
“Watanzania wasiwe na shaka yoyote, wanajeshi wamejipanga vizuri na
kwa uhakika na kama ilivyo ahadi yao, wapo tayari kulinda nchi yetu
mpaka tone la mwisho la damu yao,” alisema na kuongeza kuwa kama
wabunge, nao wameridhika na maandalizi ya jeshi, kwani wapo imara na
timamu.
Alisema serikali haitaki kufika huko, kwani wakati wa Vita ya Uganda
mwaka 1978, wananchi waliumia na kwamba kama nchi, inafahamu athari za
vita kiuchumi na kwa maisha ya binadamu.
“Hatutaki kufika huko kwani si jambo jema, ndiyo maana tunasema
tumalize kwa njia ya mashirikiano na kwa mazungumzo ya kidiplomasia ya
mawaziri wanaohusika ikishindikana tutafute msuluhishi,” alisema.
Mwaka 1978, Tanzania iliwahi kuingia katika vita na Uganda, baada ya
aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Iddi Amin Dada, kuvamia sehemu ya Tanzania
na kudai kuwa ni yao.
Juzi, Membe alitoa tamko la serikali na kuyataka makampuni yote
yanayoendelea kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa hilo kuondoka mara
moja pamoja na Serikali ya Malawi kuheshimu mazungumzo yaliyofikiwa.
Alisisitiza eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo Tanzania.
Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
kuzipiga marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na
ndege tano zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote
zinazoendelea na shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara
moja kuanzia leo Jumatatu,” alisema Membe na kuongeza kuwa, Serikali ya
Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote.
Alisema kwa kuzingatia nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa
Kiingereza mwaka 1928 na 1938, zinaonesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo
katikati.
Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa
kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo kati ya
Cameroon na Nigeria.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment