Na Imelda Mtema
NDOA ya mwanamitindo Jacqueline Patrick ‘Jack’ na mumewe Abdulatifu Fundikira a.k.a Tiff ipo hatarini kuvunjika na habari kutoka jikoni ni kwamba, sasa Jack amevua pete ya ndoa na kubaki na ile ya uchumba.
Jack amefanya kitendo hicho, wakati mumewe akila msoto nyuma ya nondo katika Gereza la Keko, Dar akisubiri kesi yake ya madai ya kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya inayoendelea katika Mahakama ya Kisutu jijini.
Mwandishi wetu alimnasa mwanamitindo huyo mrembo, juzikati, jijini Dar es Salaam, akijivinjari bila pete ya ndoa, ndipo alipomuuliza na kumpa majibu ya kushangaza kama siyo ya kushtusha.
SIKIA SABABU ZAKE
“Najua wengi wanaweza kunishangaa wakiniona sina pete yangu ya ndoa, lakini nataka kusema kwamba nipo sahihi na ninajua ninachokifanya. Kwa sasa ni kama sina ndoa au ndoa ipo nusu nusu.
“Siyo makosa nikisema kuwa, naona kama niko mguu ndani mguu nje. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyonifanya niamue kuvua pete yangu ya ndoa,” alisema Jack na kuongeza:
“Unajua mume wangu yupo kwenye matatizo sasa hivi (gerezani) na sijui nini cha kufanya. Kifupi nipo katika wakati mgumu sana, ndiyo maana nimefikia uamuzi wa kuondoa pete kidoleni mwangu.
“Nahisi kama inazidi kuniongezea machungu moyoni mwangu. Sioni faida ya kuivaa kabisa. Afadhali nibaki na hii ya uchumba.”
PEKUPEKU MITAANI
Risasi Mchanganyiko lilifanya uchunguzi wake kimya kimya mitaani na kupata picha tofauti na aliyoieleza Jack.
Chanzo chetu makini, kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, kilitupenyezea habari kwamba, tangu Tiff apelekwe mahabusu katika Gereza la Keko, uhusiano kati ya wawili hao umelegalega.
“Kwanza Jack hajaenda kumuona mumewe hata siku moja...unajua hawa bwana, ugomvi wao haukuanza juzi, ni kabla jamaa yake hajapata matatizo. Sidhani kama kuna ndoa tena pale...na hivi mumewe yupo sero ndiyo kabisa,” kilipasha chanzo chetu.
Kikaongeza: “Jaribuni kufuatilia zaidi, lakini wale kuendelea tena, sidhani kama itawezekana kwa hali waliyofikia.”
SAUTI YA FUNDIKIRA KUTOKA KEKO
Gazeti hili lilifunga safari hadi katika Gereza la Keko, Dar kwa lengo la kumtembelea Abdulatifu ikiwa ni pamoja na kufuatilia habari hii.
Huyu hapa anazungumza: “Mke wangu hajafanya kitu kizuri. Inaniuma sana kusikia kwamba amevua pete ya ndoa. Jambo hilo linaninyima amani sana. Mimi kupata matatizo siyo sababu ya msingi ya yeye kuvua pete. Kwa kweli imeniuma sana.”
No comments:
Post a Comment