MWANDISHI WETU
HUKU akisubiri hatma yake kwenye Kamati ya Ligi, staa wa Simba, Emmanuel Okwi wa Simba amemliza mlemavu wa miguu, Jumanne Bongoya 'J4' baada ya kumpiga na chupa ya maji jukwaani alipokuwa amekaa wakati alipotolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo na sasa suala hilo linatinga polisi.
'J4' ametoa taarifa ya tukio hilo katika Kituo cha Polisi Chang'ombe jijini Dar es Salaam. Okwi ambaye ni raia wa Uganda na mchezaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo 'The Cranes', alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 38 na mwamuzi Andrew Shamba katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu waliposhinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kumpiga kiwiko, Kessy Mapande, Jumatano iliyopita.
Alipokuwa akitoka nje ya uwanja, alirusha chupa ya maji katika jukwaa la Yanga na kumpiga mlemevu huyo. Akizungumza na Mwanaspoti, J4 alisema: "Nimeshangazwa na kitendo cha Okwi kunipiga na chupa ya maji kwenye mbavu si cha kiungwana na uanamichezo ukizingatia yeye ni staa. "Waliokuwa wanazomea ni wengine sikuhusika kabisa, unajua tukio lile sikuwa nalo makini, nilikuwa nimeduwaa baada ya kusikia timu yangu (Yanga) imefungwa mabao 3-0 na Mtibwa, ndiyo nikasikia chupa imenipiga.
"Iliniuma na sikuvumilia, saa 3.00 usiku, nilikwenda kutoa taarifa Polisi Chang'ombe, nikapewa PF3 kwa ajili ya kwenda kuchunguzwa hospitali." Alisema kuwa jana Ijumaa alikuwa akishughulikia suala hilo ili amchukulie RB. Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilidai kuwa linasubiri taarifa ya kamishna wa mchezo huo ili walifanyie kazi.

No comments:
Post a Comment