KOCHA Tom Saintfiet amejifananisha na Alex Ferguson wa Manchester United, lakini Yanga italazimika kumlipa zaidi ya Sh 200 milioni sawa na dola 130,000.
Kocha aliyetimuliwa na Yanga, Tom Saintfiet
Katika mkataba wa miaka miwili kocha huyo aliosaini Julai 6 mwaka huu na Yanga analipwa dola 6,500 (zaidi ya Sh 10 milioni) kwa mwezi na tayari alilipwa taslimu mshahara wa kuanzia Julai mpaka Oktoba jambo ambalo linamfanya adai mishahara ya miezi 20. Yanga ndiyo iliyositisha mkataba huo ambapo kwa mujibu wa sheria za kazi watalazimika kumlipa miezi 20 iliyobaki ambayo ni Sh 201,500,000 milioni.
Kocha huyo aliiambia Mwanaspoti jana Jumamosi kwa kifupi kwamba hatambui kusimamishwa kwake kwa vile hadi mchana alikuwa hajapewa barua rasmi zaidi ya kusikia kwa watu. "Kulikuwa na kikao kifupi jana (juzi Ijumaa) usiku na uongozi pamoja na wachezaji walikuja hapa hotelini kwangu (Protea-Masaki) kukaibuka majibizano ya hapa na pale na kutoleana lugha chafu na hakikuisha kwa amani.
"Siwezi kuzungumza sana yaliyojiri waambie viongozi watasema. Lakini sikupendezwa na mambo yaliyotokea, nasikia nimesimamishwa lakini sijapewa barua rasmi wala sina taarifa ninachojua ni kwamba kulitokea kutokuelewana kati yangu na kiongozi mkubwa na tukajibizana sana. "Mwulize yeye atakuambieni alifanya nini, mwulizeni yule dikteta atasema. Wanafanya mambo ambayo siyaelewi kabisa ndiyo maana siwezi kuzungumza kiundani sana hili suala, lakini kama wametangaza kwamba wamenifukuza mimi nasubiri nione nini kitatokea.
"Niliridhia kuja Yanga kwavile niliona ni sehemu salama ambayo naweza kufanya kazi na kuipa mafanikio makubwa zaidi lakini mambo yamekuwa magumu na nasikitikia mashabiki ambao niliwapenda na walinipa sapoti kubwa mimi na timu ndiyo maana Kombe la Kagame hatukulikosa. "Nilitaka kuwapa makombe zaidi kama zawadi na fadhila kwao na heshima ya klabu, tumekuwa kwenye kipindi kigumu hivi karibu lakini hiyo hali ndiyo ilikuwa inaelekea ukingoni. Yanga itaanza kushinda kuanzia sasa tumefanya maandalizi mazuri ambayo hata kama nisipokuwapo mimi, Minziro anaweza kuipa timu ubingwa.
"Yanga itakuwa bingwa msimu huu, haya mambo yanayotokea ni ya kawaida kwenye maisha ya soka," alisisitiza kocha huyo mwenye miaka 39 ambaye uongozi umedai kuwa ana kiburi na ni mkaidi kutii maagizo ya mabosi wake.
AJIBU MAPIGO
Uongozi wa Yanga umedai kuwa kocha huyo haambiliki na hataki kambi ya muda mrefu, lakini yeye amejibu. "Mimi ndiye kocha wa Yanga na ndiye ninayewajibika kutoa uamuzi wa kiufundi kwa vile ninawajibika kwa kila kitu kinachotokana na matokeo yake. Uongozi hauwezi kunilazimisha niweke kambi wapi na ya aina gani, mimi ndiye kocha. Hata Manchester United huwa hawampangii kocha Ferguson jinsi ya kuweka kambi na kuishi na wachezaji wake kambini.
Ana mipangilio yake ya kazi kuhusu kambi na huwa uongozi wa juu haumungilii na ndio utaratibu unaofanywa na makocha wote dunia, uongozi haupangi kambi hiyo, ni kazi ya Kocha Mkuu na benchi lake la ufundi. "Mimi ni kocha msomi na mwenye taaluma yangu najua nini cha kufanya na miiko ya kazi yangu naijua, mimi ni profesheno huwezi kunipangia mpaka jinsi ya kuweka kambi. Ni jukumu langu na naweka kambi kutokana na aina ya mechi niliyonayo na ni kitu cha kukumbushana tu na kuwaweka wachezaji kwenye utulivu wa muda mfupi kabla ya mechi.
"Huwezi kumweka mchezaji kambini muda mrefu ukijiandaa na mechi moja ya ligi, mazoezi ninayowafanyisha ni ya hali ya juu sana na ninamwamini kila mmoja nikijua kwamba anajitambua," alisema kocha huyo huku akikana ukaidi wake. Mwanaspoti ilizungumza na kocha huyo saa tano asubuhi jana Jumamosi akikuwa kwenye taxi na mchumba wake wakielekea ufukweni kujipumzisha na kula wikiendi huku akionekana mwenye mawazo.

No comments:
Post a Comment