Hussein, ambaye alikuwa mfanyakazi wa ndani wa Dkt. Assery Mchomvu anayeishi Tegeta, Dar es Salaam, alikumbwa na mauti hayo juzi mchana nyumbani kwa daktari huyo.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu tukio hilo, Dkt. Mchomvu alisema siku ya tukio alichelewa kwenda kazini kama ilivyo kawaida yake na wakati Hussein anamtayarishia kifungua kinywa, alimwuliza akitaka kujua inakuwaje mtu anapoambiwa kuwa ana ugonjwa wa zinaa, “Nilimjibu kuwa maana yake ni kwamba mtu huyo amefanya mapenzi bila kinga na atakuwa ameambukizwa magonjwa hatari ya zinaa, lakini tiba yake ni kuwahi hospitali kutibiwa,” alisema daktari huyo.
Alisema baada ya jibu hilo, mfanyakazi wake huyo alionekana kuridhika na kuendelea na kazi, na saa saba mchana akiwa kazini, alipigiwa simu na mfanyakazi wake mwingine wa bustani, Shafii, ambaye alimtaarifu kuwa Hussein amekunywa sumu.Alisema alishitushwa na taarifa hizo na kumtaka kijana wake huyo atoe taarifa kwa majirani ili wamsaidie kumpa huduma ya kwanza, lakini pia kumwahisha hospitali ya jirani Tegeta ili kuokoa maisha yake.
Dkt. Mchomvu alisema kijana huyo, alipewa huduma ya kwanza ya kupewa maziwa na kukimbizwa hospitali ya Mico, Tegeta ambako walibaini kuwa alikunywa kemikali zisizofahamika na kujaribu kumsafisha tumbo, “Hata hivyo, kwa kuwa alikunywa kiasi kikubwa cha dawa ya kuulia wadudu ilishindikana kuokoa uhai wake na alifariki dunia,” Alisema waliporejea nyumbani, Shafii aliwaonesha kikopo cha dawa ya kuulia wadudu inayotumiwa kunyunyizia katika nyumba kikiwa kitupu ambapo walibaini pia kuwa marehemu alikunywa vikombe viwili vya dawa hiyo.
Aidha, alisema walipokagua chumbani kwa kijana huyo walikuta ujumbe aliouandika kwa ndugu, jamaa na marafiki zake, akiwaeleza kuwa wamwombee aendako kwani amepima ili kujua kama ameathirika na UKIMWI na kukutwa ameathirika, “Hata hivyo, cha kushangaza, pembeni ya ujumbe huo tulikuta cheti alichokwenda kupima ugonjwa huo ambacho kinaonesha kuwa ni negative (hajaathirika),” alisema.Alisema alipomhoji Shafii alisema juzi asubuhi alimsikia Hussein akiwapigia simu ndugu zake kijijini kuwataarifu kuwa amepima Ukimwi na kubainika kuwa hajaathirika, hata hivyo walipomhoji cheti kimeandikwa nini, aliwajibu ‘negative’, na kumwambia kuwa maana yake ni kwamba ameathirika.Alisema mwili wa marehemu unafanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Kairuki na baada ya hapo utasafirishwa kwa ajili ya maziko kijijini kwao Singida.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea tukio hilo akisema Hussein alikunywa dawa ya kuulia wadudu aina ya Nuvari 500 CC baada ya kupata hofu kuwa ameathirika na UKIMWI, “Nachukua fursa hii kuwaasa wananchi kuacha kuchukua uamuzi wa haraka hasa wa kukatisha maisha yao, kwani pamoja na kwamba ni dhambi kufanya hivyo, pia ni kinyume cha sheria,” Alisema endapo Hussein angekuwa na subira, angebaini ukweli kuwa neno ‘negative’ halimaanishi kuwa ameathirika na hata kama angeathirika, angeweza kuishi kwa muda mrefu kuliko uamuzi wake wa kukatisha ghafla maisha yake.Habari imeandikwa na Halima Mlacha via HabariLeo
No comments:
Post a Comment