Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, ameingia matatani baada ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kumwandikia barua ya kumtaka atoe maelezo kwanini ameshindwa kuwalipa fidia wakazi tisa wa eneo la Kangae B kiwanja Na. 240 kitalu “EE” jijini humo waliobomolewa nyumba zao bila kuwapa taarifa.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe.
Barua ya wizara hiyo yenye kumbukumbu namba LD/146519 Vol. V/23 iliyoandikwa Juni 23, mwaka huu na kusainiwa na Anna Mdemu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, ikimtaka Mkurugenzi huyo atoe maelezo ya kina ya suala hilo.
Barua hiyo ambayo NIPASHE imeiona, imeeleza kuwa kulikuwepo na ukiukwaji mkubwa wa taratibu wakati wa ubomoaji na kumilikisha kiwanja hicho na hivyo kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Ilemela iliamulu wananchi hao walipwe fidia kutokana na hasara waliyoipata.“Wizara inahitaji kupata taarifa kamili juu ya mgogoro huo na kiini cha mgogoro na ni kwa nini hamjawalipa fidia wananchi hao kama ilivyoazimiwa kwenye kikao cha ulinzi na usalama cha wilaya,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.Naye Mkurugenzi wa Jiji hilo, Kabwe alipoulizwa ni kwa nini amekaidi agizo la wizara la kuwalipa fidia wakazi hao, alijibu kwa kifupi kuwa wakazi hao walivamia eneo hilo na walijenga kinyume cha sheria kisha kukata simu.Kamishna wa Ardhi wa Wizara hiyo, Anna Mdemu, alithibitisha kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi hao na kusema kuwa walimwandikia barua Kabwe kutaka kutolea ufafanuzi juu ya mgogoro huo.“Ni kweli tulipokea malalamiko hayo, lakini suala hilo kwa sasa lipo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba Maendeleo ya Makazi,” alisema Mdemu.Mmoja wa waathirika wa bomoabomoa hiyo, Mussa Maduka, alisema Juni 23, 2009 majira ya mchana, Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiongozwa na Kabwe ilitumia mabavu ya kubomoa nyumba hizo bila kuwapa taarifa ya kuondoka eneo hilo wala kupewa fidia.Alisema kufuatia hali hiyo, walitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa naye akamwagiza Mkuu wa Wilaya ashughulikie suala hilo kupitia Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya na Novemba 13,2009 walisomewa na Mkuu wa Wilaya maamuzi yalioyotolewa na kamati hiyo mojawapo likiwa ni kuitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Ardhi ilipe fidia wanachi tisa waliobomolewa nyumba hizo.
Alisema maamuzi mengine ni kuwa wananchi waliobomolewa warudishiwe eneo hilo na waliohusika na ubomoaji huo wawajibishwe mara moja maana haki na utawala bora haukuzingatiwa.Maduka alisema kipindi kirefu kilipita pasipo maamuzi hayo kufanyiwa kazi ndipo walimuandikia barua aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa wakati huo, John Chiligati, ili awasaidie kudai haki yao.Alisema tangu mwaka huo hakuna msaada wowote walioupata kutoka katika uongozi wa serikali badala yake walikuwa wanazungushwa huku mwafaka wa kumaliza kwa mgogoro huo ukikwama.Alisema Juni 6, mwaka huu waliamua kulifikisha suala hilo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, ambaye aliandika barua iliyosainiwa na Mdemu ya kumtaka Mkurugrnzi wa Jiji la Mwanza Kabwe awalipe fidia wakazi hao.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment