HATIMAE mwimbaji maararufu wa muziki wa dansi, Mwinjuma Muumin ameihama rasmi Twanga Pepeta.
Akiongea
na saluti5 usiku wa jana kuamkia leo, mwimbaji huyo alisema kwa nia
njema kabisa bila ugomvi wala mgogoro wowote ameihama Twanga Pepeta na
kujiunga na bendi changa ya Victoria Sound yenye maskani yake jijini Dar
es Salaam.Muumin amesema kesho Jumatano atakwenda Idara ya Habari (Maelezo) kuongea na Waandishi wa habari.

Mapema
jana mchana saluti5 ilimtembelea Muumin nyumbani kwao Bagamoyo (kama
picha zinavyoonyesha hapo juu) ambapo licha ya kuongea mengi lakini
alikataa kuzungumzia uvumi uliozagaa kuhusu kuhama kwake Twanga Pepeta.
“Mimi
hadi muda huu bado ni mwanamuziki wa Twanga ila baadae nitakuja town
(Dar es Salaam), tutafutane usiku pengine nitakuwa na kitu tofauti cha
kukueleza” alisema Muumin katika maongezi yake na saluti 5 jana mchana.
Hatimae
saluti5 ikakutana tena na Muumin saa 6:45 jana usiku jijini Dar es
Salaam na ndipo alipoweka mambo hadharini kuwa ameihama rasmi bendi
aipendayo sana ya Twanga Pepeta.
“Ni uamuzi mgumu sana, naipenda Twanga Pepeta, nilipata malezi mazuri kuanzia kwa uongozi, wanamuziki, maseneta hadi mashabiki.
“Kibinaadamu
najua ziko sehemu kadhaa ambazo tulikwazana lakini sitapenda mazuri
mengi niliyoyapata pale yafunikwe na mabaya machache, itakuwa ni ukosefu
wa fadhila, naomba wote watakaoumizwa na kuhama kwangu wanisamehe na
tulindiane heshima.
“Haitakuwa
jambo jema mimi au Twanga Pepeta tukaanza kupita huku na kule na
kuchafuana, bado naichukulia Twanga na Aset kwa ujumla kama nyumbani
kwangu” alisema Muumin.
Alipoulizwa
ni kwanini ameihama Twanga wakati aliahidi kumalizia muziki wake
kundini hapo, Muumin alisema amezingatia vitu viwili.
Kwanza
ni dau alilopewa Victoria Sound, pili ni uchanga wa bendi aliyojiunga
nayo. “Naiona Victoria kama bendi changa ambayo haitaweza kuwa bendi
shindani kwa Twanga Pepeta, kamwe nisingethubutu kujiunga na bendi
yeyote shindani kwa Twanga” alisema Muumin aliyetunga wimbo Penzi la
shemeji katika albam ya Dunia Daraja.
Aidha,
Muumin aliongeza kuwa anaamini kuwa kuondoka kwake Twanga Pepeta
hakutaacha pengo lolote kwa vile ina mkusanyiko wa wanamuziki wenye
vipaji vya hali ya juu.
Muumin
amesema changamoto aliyonayo sasa ni ya kutengeneza nyimbo nzuri kwa
bendi yake mpya ili kuitoa katika hatua moja kwenda hatua nyingine.
Kuondoka
kwa Muumin Twanga Pepeta kunahitimisha wingu zito lililokuwa limetanda
kufuatia kutoonekana kwake jukwaani wiki nzima iliyopita.
CHANZO CHA HABARI SALUTI5
No comments:
Post a Comment