MAHAKAMA ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, imewahukumu kifungo
cha maisha vijana wawili kwa makosa mawili ya ubakaji na kumuambukiza
ugonjwa wa ukimwi mtoto wa miaka minne.
Akitoa hukumu hizo kwa nyakati tofauti, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
mahakama hiyo, Ushindi Swalo, alisema mahakama imeridhishwa na ushahidi
uliotolewa huku mmoja wa watuhumiwa hao akikiri kutenda kosa hilo la
kumbaka mtoto wa miaka minne.
Katika tukio la kwanza, Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo, Zephania
Mnisi, alisema kuwa Desemba 21 mwaka jana, mshitakiwa Revocatus Mihayo
(25) alimbaka mtoto wa miaka minne katika Kijiji cha Msonga wilayani
Bukombe.
Mnisi aliiambia mahakama hiyo kuwa katika tukio hilo, Mihayo
alikamatwa akiwa amempakata mtoto huyo mapajani, huku akimbaka na
uchunguzi wa awali wa daktari ulionesha alikuwa ameharibika sehemu zake
za siri.
Alisema wakati kesi hiyo ikiendelea na miezi kadhaa ikipita, mtoto
huyo alifanyiwa uchunguzi wa daktari kwa mara ya pili na kubainika
tayari ameambukizwa virusi vya ukimwi, shitaka ambalo liliongezwa kwenye
kesi yake ya msingi ya ubakaji.
Katika shtaka la pili, Shija Marko (18) mkazi wa Lulembera anadaiwa
kumbaka mtoto wa miaka minne baada ya kukutana naye shambani wakati
mtuhumiwa akiwa na shughuli za kilimo.
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa, katika tukio
hilo mtoto huyo alipita shambani kwa Marko akiwa uchi wa mnyama jambo
ambalo kijijini ni kawaida, lakini mshitakiwa alimshika na kumlaza
kwenye matuta na kuanza kumbaka.
Hata hivyo mshitakiwa Marko alikiri papo hapo kutenda kosa lake na
kumfanya hakimu Swalo, amhukumu kifungo cha maisha kwa kosa hilo.
Akitoa adhabu hizo kwa nyakati tofauti kwa washtakiwa hao wawili,
Mihayo na Marko, hakimu Swalo alisema kwa kuwa washitakiwa wametenda
makosa ya kubaka watoto chini ya umri wa miaka kumi, kifungo cha miaka
30 na viboko 12 kimejifuta na sasa watatumikia kifungo cha maisha ili
liwe funzo kwa vijana wengine.
No comments:
Post a Comment