Rais Jakaya Kikwete amezindua Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela na kusisitiza kuwa ni lazima Tanzania iwekeze kikamilifu kwenye sayansi na teknolojia.Alisema ni lazima kutumia sayansi ili nchi iweze kuzitumia rasilimali zake ipasavyo na kujiletea maendeleo kama ilivyotokea kwa mataifa yaliyoendelea.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa chuo hicho kilichoko jijini Arusha ambacho licha ya kuzinduliwa, kilianza kutoa shahada za Uzamili na Uzamivu kuanzia mwaka jana.
Alisema nchi zilizoendelea zimewekeza katika sayansi na teknolojia kwa sababu bila sayansi hakuna linaloendelea zaidi ya kupigia kelele.
“Lazima tuwekeze katika vyuo hivi vya utafiti wa sayansi na teknolojia ili tuweze kuendelea hasa sisi nchi maskini, ili tuwe kama wenzetu walioendelea,”alisisitiza.
Alisema iwapo Tanzania itaweza kuziba pengo la masula ya sayansi na teknolojia, itaweza kupiga hatua katika tafiti mbalimbali za rasilimali zilizopo, bila kutegemea wataalamu wa nje.
Kikwete alisema kupitia chuo hicho, Tanzania itaweza kupata ufumbuzi wa changamoto zinazokabili nchi katika masula ya utafiti mbalimbali.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu hiyo ndiyo maana katika miaka saba ya uongozi wake, ameendeleza elimu kwa asilimia 97 na kutoa kipaumbele kwenye wanafunzi wanaosomea masomo ya sayansi.
Kikwete aliiagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kujenga barabara ya lami na kubwa itakayowezesha kutumiwa na wateja wa Chuo cha Nelson Mandela.
Ufunguzi huo ni mwendelezo wa ziara yake Jijini Arusha, baada ya kuzindua Jiji juzi na kuweka jiwe la msingi katika barabara zinazojengwa mkoani hapa.
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Bilali, ambaye ndiye Mkuu wa Chuo hicho, alisema ataendelea kushirikiana na bodi ya chuo hicho, pamoja na walimu ili kuweza kutoa elimu bora na pia kubuni mbinu zitakazowawezesha kupata mapato na kupelekea chuo hicho kujiendesha.
Makamu Mkuu wa Chuo Profesa, Burton Mwamila, alisema chuo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kufanya tafiti katika maeneo ya sayansi na teknolojia ambapo wameanzisha ushirikiano wa utoaji wa elimu na vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment