VIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho, Sheikhe Faridi Hadi Ahmed na
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sheikh Mselem Ali Mselem, wamewasilisha
maombi Mahakama Kuu ya Vuga Zanzibar, kutaka kufungua kesi kupinga
kunyolewa ndevu wakiwa mahabusu.
Kutokana na ombi hilo, Mahakama Kuu ya Vuga mjini hapa, imekubali
ombi hilo na kutoa uamuzi wa kuwaruhusu viongozi hao, wafungue kesi ya
madai, kupinga kunyolewa ndevu zao na kutotendewa haki wakiwa mahabusu.
Sheikh Farid na wenzake, wanashtakiwa kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa taifa.
Uamuzi wa kuwaruhusu viongozi hao wafungue kesi ya madai, umetolewa
jana na Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, George Kazi, baada ya
kupitia kwa makini maombi ya watuhumiwa hao.
Washtakiwa hao waliwasilisha mambo hayo Novemba 8, mwaka huu, kupitia
kwa mawakili wao, wakipinga kitendo cha polisi kuwanyoa ndevu na
kutowatendea haki wakiwa mahabusu.
Maombi hayo yaliwasilishwa na washtakiwa wanane, akiwemo Sheikh Farid na Mwenyekiti wa Uamsho, Sheikh Mselem.
Wengine katika kesi hiyo ni Mussa Juma Issa, Suleiman Juma Suleiman,
Azan Khalid Hamdan, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman na Ghalib
Ahmada Omar.
Akitoa uwamuzi wa kufungua kesi ya kupinga kunyolewa ndevu, Jaji Kazi
alisema watuhumiwa wana haki ya kufungua kesi mahakama kuu juu ya kile
wanachokilalamikia na kwamba mahakama kuu itakuwa na uamuzi wa
kuyasikiliza madai yao tofauti na kesi ya msingi ya uchochezi na
kuhatarisha amani.
Kupitia kwa mawakili wao, watuhumiwa hao walidai kuwa wananyimwa uhuru
na haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kupigwa marufuku kufuga ndevu
wakiwa rumande ya Chuo cha Mafunzo (Magereza).
Katika kesi yao ya msingi, watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka
manne yakiwemo ya kutoa lugha za uchochezi, kufanya vurugu na
kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara mjini Zanzibar.
Wakizungumzia kesi ya msingi kwa watuhumiwa hao, waendesha mashtaka wa
serikali walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamili na kwamba
wanaomba siku nyingine ya kutajwa.
Mrajis huyo wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, itakapotajwa tena.
Kama kawaida, Jeshi la Polisi lilifunga barabara zote za kuingia na
kutoka mahakamani na kuimarisha ulinzi ndani na nje ya mahakama hiyo
ambapo kila pembe walionekana makachero wa polisi na Askari wa Kikosi
cha Kutuliza Ghasia (FFU), wenye silaha za moto.
Baadhi ya wananchi waliofika mahakamani hapo, waliwataka waandishi wa
habari kuandika ukweli kuhusiana na kesi hiyo ili kuinusuru nchi na
machafuko.
Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea, Salum Toufik na
Abdallah Juma Kaka, huku upande wa serikali ukiwakilishwa na Ramadhan
Nassibu na wenzake wawil.VIA Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment