MSAFARA wa timu ya Yanga uliokuwa ukielekea jijini Tanga, jana ulivamiwa na kundi la wahuni ambao walilivurumishia mawe basi lao na kupasua vioo vilivyomjeruhi mchezaji mmoja katika eneo la Kabuku, Handeni.
![]() |
Dereva wa basi la Yanga Maulid Kiula akionyesha sehemu ambayo kioo kimevunjwa na watu wasiojulikana ktk kijiji cha kwedikwazu wkt time ikipita kijijini hapo kwenda jijini Tanga. |
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Laurence Mwalusako, alisema msafara huo wenye wachezaji 18 na viongozi saba, walikumbana na sakata hilo majira ya saa sita mchana.
Mwalusako alisema kutokana na tukio hilo, mchezaji Simon Msuva alipata majeraha madogomadogo mara baada ya kioo kilichopasuka kumwangukia.
“Vijana wetu wamekumbana na ghasia hizo maeneo ya Segera, mara baada ya wahuni kuliponda gari mawe na kupasua kioo; na Msuva kuumia,” alisema Mwalusako.
Naye meneja wa timu hiyo, Salehe Hafidhi, alisema mara baada ya kukumbana na kashkashi hiyo, walikwenda moja kwa moja katika kituo cha polisi cha Kabuku na kutoa taarifa juu ya fujo walizofanyiwa.
“Hivi sasa tunatoka polisi ila tunamshukuru Mungu vijana wangu hawajaumia kutokana na ghasia hizo na sasa tumeanza safari yetu ya kwenda Tanga,” alisema Hafidh.
Kwa upande wake, Msuva alisema ameumia kidogo usoni mara baada ya kioo kumwangukia, ila anamshukuru Mungu anaendelea vizuri na hajapata majeraha makubwa.
Kutokana na ghasia hizo, uongozi wa Yanga umeliomba Jeshi la Polisi, kuwafuatilia wale wote ambao wamefanya uharibifu huo ili waweze kuwachukulia hatua zaidi za kisheria ili tataizo hilo lisije likajitokeza tena.
No comments:
Post a Comment