WILAYA ya Bariadi mkoani Simiyu, imetajwa kuwa ni miongoni mwa
wilaya zinazoongoza kwa wanafunzi wake kuacha masomo na kwenda kuuza
pombe za kienyeji na hivyo kuporomoka kwa elimu wilayani humo.
Mbali na hayo, imeelezwa kwamba ajira za utotoni, baadhi ya viongozi
wa vijiji kutosimamia vema shughuli za kimaendeleo katika maeneo yao,
ushirikiano mbovu baina ya watendaji na wananchi na makato makubwa ya
mishahara ya walimu, ni chanzo kikuu cha kukwamisha maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi mjini Bariadi na walimu kutoka sehemu
mbalimbali wanaoshiriki warsha ya siku tatu ya 'Chukua Hatua',
iliyoandaliwa na Taasisi ya Kutetea na Kujenga Demokrasia na Utawala
Bora (ADLG).
Wakichangia mada ya kero katika sekta ya elimu, walimu hao walisema
wanafunzi wengi wamekuwa wakiacha masomo kisha kujihusisha na biashara
ya uuzaji wa pombe, jambo linalodidimiza ukuaji wa maendeleo ya sekta
hiyo.
Kwamba hata baadhi ya viongozi wa ngazi za vijiji na wizara husika
wameonekana kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wa wanafunzi
hao.
Walisema kuwa ili kuondoa tatizo hilo na hatimaye wilaya hiyo kupiga
hatua kubwa za kimaendeleo, ni vema viongozi wa ngazi zote
wakashirikiana pamoja kupambana na hali hiyo mbaya, ikiwa ni sambamba na
kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi ama walezi wanaoshindwa
kusimamia maendeleo ya elimu kwa watoto wao.
“Wanafunzi wengi wanaingia darasani wakiwa na njaa. Kwa maana hiyo
uelewa unakuwa mdogo sana, maana wengi wanasinzia na kushindwa kusoma
vizuri,” alisema mmoja wa walimu hao.
Aidha walimu hao walikwenda mbali zaidi na kusema kwamba hulka ya
baadhi ya wazazi na walezi kuwaoza watoto wao wa kike, unywaji wa pombe
baina ya walimu wakati wa kazi ni kikwazo pia cha upatikanaji wa
maendeleo, na kwamba baadhi ya wananchi wa vijiji husika wamekuwa
wakiendekeza ubaguzi wa kabila kwa walimu.
Awali, Mkurugenzi wa ADLG, Jimmy Luhende, alisema lengo la warsha hiyo
ni kuwapatia elimu ya uwajibikaji walimu wa shule mbalimbali katika
wilaya sita za mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Geita.
Habari na Sitta Tumma, Bariadi.
No comments:
Post a Comment