Na Edson Kamukara
UKOSEFU wa umakini serikalini, umeendelea kuliingiza taifa
kwenye gharama zisizo za msingi ambapo sasa mahakimu wakazi 370
wanalazimika kulipwa mishahara bila kufanya kazi, Tanzania Daima
limebaini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa mahakimu wakazi 300
waliajiriwa Juni mwaka huu katika ajira mpya kwa masharti kwamba
wangefanya kazi kwenye mahakama za mwanzo.
Baadaye Septemba mwaka huu, mahakimu wengine 70 waliapishwa na
kupandishwa kutoka mahakama ya mwanzo kuwa mahakimu wakazi na hivyo
kufanya idadi yao kufika 370 ambao hulipwa takribani sh 700,000 kila
mmoja kwa mwezi.
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kama kukosekana kwa umakini
katika utendaji serikalini, sheria iliyopo sasa kuhusu utendaji wa
mahakimu hao ilipaswa kufanyiwa marekebisho kwanza kabla ya wao
kuajiriwa.
Kwa mujibu wa sheria ya sasa ya mahakimu na mahakama sura namba 11
kifungu cha sita, ni kwamba hakimu mkazi hana mamlaka ya kukaa katika
mahakama ya mwanzo bali mahakama ya wilaya na ya hakimu mkazi (mkoa).
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya mahakimu hao waliilalamikia
serikali kwa kukurupuka kuwapa ajira bila kufanyia marekebisho sheria,
na hivyo kuhoji ni kwanini wasipangiwe kazi kwenye mahakama zenye hadhi
yao hadi sheria itakapokuwa imebadilishwa.
“Kwa kweli kitendo hiki cha kulipwa mshahara pasipo kufanya kazi ni
kama kuhujumu uchumi wa nchi, lakini pia serikali imeamua kuharibu
taaluma zetu,” kilisema chanzo chetu.
Kwa sasa mahakimu hao wanaripoti tu kwenye vituo vyao vya kazi na
kusaini kitabu cha mahudhurio kisha kuondoka kwa vile hawana kazi
maalumu ya kufanya katika mahakama hizo.
“Mikoa kadhaa kama Mwanza na Pwani, majaji wenye uelewa wanawapangia
kazi mahakimu hawa kwenye mahakama stahiki. Lakini bado si maeneo yote
wanafanya hivyo.
“Serikali ni kweli ilikuwa na nia njema ya kuboresha mfumo wa mahakama
ili hawa wasomi wahudumie huko, lakini kwanini wasirekebishe sheria
kwanza?” kiliongeza chanzo hicho.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe pamoja na Naibu wake,
Angela Kairuki hawakuwa tayari kupokea simu na hata walipoandikiwa
ujumbe mfupi wa maneno vile vile hawakujibu, hivyo juhudi za kuwatafuta
ili wafafanue zinaendelea.
No comments:
Post a Comment