Watoto watatu wa familia moja wamekufa baada ya kuugua ghafla ugonjwa usiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai alisema kuwa watoto hao walikufa Oktoba 30 mwaka huu saa 7 wakati wanapatiwa matibabu katika Zahanati ya Kijiji cha Kasongati kichipo Wilaya ya Kakonko.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Yudines Wilbart (6), Abela Wilbaet (4) na Ukiwa Wilbart (2). Alisema polisi wanaendelea kuchunguza ili kubaini chanzo cha vifo vya watoto hao.
Katika tukio jingine; Watoto wawili wamefariki dunia jijimo Mwanza, akiwamo aliyekufa wakati akitolewa mimba kwenye zahanati iliyoko eneo la Kilimahewa, Kata ya Nyamanoro.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, amesema ofisini kwake jana kuwa matukio hayo yalitokea kwa nyakati tofauti kati ya Oktoba 28 na 31, mwaka huu
Alisema tukio la kwanza lililotokea Oktoba 28 linamhusisha Jacqueline John (15), aliyekuwa akiishi na wazazi wake wote wawili, alifariki dunia saa 3.00 usiku wakati akitolewa mimba na daktari wa zahanati hiyo.
Alisema Daktari huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Alisema pia mtoto mwenye umri wa miezi mitatu, Ashifat Abdisalama, alifariki dunia juzi saa 4.00 asubuhi, katika eneo la Mlima ‘B’, Kata ya Kirumba, baada ya kuangukiwa na ukuta wakati akiwa amelala ndani na wazazi wake, Abdisalama Hussein (3) na Nadia Gereshani (25) wakati mvua kubwa zikinyesha.
Alisema majeruhi wote watatu walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, lakini mtoto huyo alifariki dunia na wazazi wake bado wamelazwa wakiendelea na matibabu.
Wakati huo huo, wanafunzi 30 wa darasa la pili na mwalimu wa Shule ya Msingi Lake jijini humo, juzi saa 4.00 asubuhi walinusurika kifo baada ya kupigwa na radi wakiwa darasani wakati mvua kubwa zikinyesha.
Matola alisema majeruhi wote walikimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa matibabu na kuruhusiwa isipokuwa Felix Revocatus (8) bado amelazwa baada ya kupata majeraha makubwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment