MABINGWA wa soka wa Kenya, Tusker FC, jana walizidi kudhihirisha
ubabe wao kwa miamba ya soka ya Tanzania, baada ya kuwabonyeza Simba
kwa mabao 3-0 kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa Uwanja
wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Tusker ambao ni mabingwa mara 10 wa Ligi Kuu ya Kenya
tangu kuanzishwa kwao mwaka 1970, wameweka rekodi ya kuvifunga vigogo
vya soka nchini baada ya kuifunga pia Yanga bao 1-0 katika mechi ya
kwanza katikati ya wiki.
Shujaa wa mechi ya jana alikuwa Ismail Dunga aliyeifungia timu yake
mabao mawili katika kipindi cha kwanza, akifunga la kwanza dakika ya 39,
baada ya kuwazidi mbinu mabeki wa Simba kabla ya kumpiga chenga kipa
William Mweta na kuujaza mpira katika vyavu.
Bao hilo liliwaamsha wachezaji wa Simba ambao walizidi kulisakama
lango la Tusker, lakini safu ya ulinzi ya Wakenya hao ikiongozwa na
Joseph Shikokoti aliyewahi kuichezea Yanga, ilikuwa makini kuokoa hatari
nyingi kumfikia kipa wao Samwel Odhiambo.
Dakika ya 45, Dunga alirejea katika lango la Simba na kumtungua Mweta kwa mara nyingine baada ya kupokea
pasi murua kutoka kwa Maurice Odipo, hivyo wakali hao kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao hayo mawili.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko hasa Simba
ambayo jana ilichezesha wageni na chipukizi, lakini Tusker walizidi
kung’ara baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 53, likifungwa kwa
kichwa na Frederick Onyango akiitendea haki kona murua iliyokuwa
imepigwa na Robert Omunuk.
Katika mechi hiyo, Simba ilifanya mabadiliko ya wachezaji mara saba saba, huku Tusker ikiwabadili sita.
Licha ya kufungwa, Simba walionesha soka maridadi huku ikiwapa picha
halisi makocha wa timu hiyo nini wafanye katika kipindi hiki cha
maandalizi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania bara na Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Mbali ya Simba na Tusker kukabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa
Afrika, pia zitakuwa visiwani Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi
litakalofikia tamati Januari 12, siku ya kilele cha maadhimisho ya
mapinduzi ya mwaka 1964.
Simba: William Mweta, Haruna Shamte, Paul Ngalewa, Hassan Hatibu,
Koman bil Keita, Mussa Mudde, Haroun Athuman, Abdallah Seseme, Abdallah
Juma, Ramadhan Chombo na Kigi Makasy.
Tusker FC: Samwel Odhiambo, Luke Ochieng, Jeremiah Bright, Mark
Odhiambo, Joseph Shikokoti, Khalid Aucho, Edwin Ombasa, Fredrick
Onyango, Ismail Dunga, Jesse Were na Robert Omunuk.
No comments:
Post a Comment