WATU 21 wanahofiwa kufa maji katika Ziwa Tangayika baada ya boti
waliyokuwa wakisafiria kutoka katika Kijiji cha Kirando wilayani Nkasi,
Mkoa wa Rukwa kuelekea Rumonge nchini Burundi kupasuka na kuzama katika
eneo la Kijiji cha Herembe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari katika eneo la
tukio, nahodha wa boti na abiria walionusurika katika ajali hiyo,
Kilimali Sefu na Muhamed Said walisema kuwa ajali hiyo imetokea jana
majira ya saa saba usiku.
Walisema jumla ya abiria 85 walikuwemo katika boti hiyo inayojulikana
kwa jina la Yarabi Salama na kati yao 64 wameokolewa na 21 wamefariki
dunia. Maiti tisa zimepatikana na 12 hazijulikani zilipo.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali
uliotokea katika eneo hilo la Herembe na kusababisha mashine ya boti
kushindwa kufanya kazi.
Boti hiyo ilikuwa imebeba idadi kubwa ya abiria na tani 45 za mihogo,
dagaa na samaki, waliokuwa wakisafirishwa kwenda Rumonge, nchini
Burundi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Herembe, Joka Mpapi na Ofisa
Mtendaji wa kijiji hicho, Adam Makuka wamelalamika kukosekana vifaa vya
uokoaji, lakini waliwashukuru wananchi kwa jitihada walizofanya za
kusaidia kuokoa.
Akizungumza na wananchi katika eneo la ajali, Mkuu wa Mkoa Kigoma,
Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya, aliwataka wananchi kuwa makini na
usafiri wa majini na kuchukua tahadhari ya kupakia mizigo na abiria
kulingana na uwezo wa boti.
“Hivi sasa kuna mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa imebadilika
sana, lazima mchukue tahadhari mnaposafirisha bidhaa zenu, mbebe abiria
na mizigo kulingana na uwezo wa boti husika,” alisema Machibya.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni.
No comments:
Post a Comment