UMATI mkubwa wa wakazi wa Jiji la Arusha, jana walijitokeza kwenye
Uwanja wa mpira wa Ngarenaro, kuadhimisha kumbukumbu ya miaka miwili ya
mauaji ya watu watatu waliouawa na polisi wakati wa maandamano ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Maandamano hayo yaliyofanyika Januari 5 mwaka 2011, yakiongozwa na
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod
Slaa na wabunge kadhaa wa chama hicho, yalilenga kupinga uvunjwaji wa
sheria, kanuni na taratibu zilizotumika kumweka madarakani Meya wa Jiji
la Arusha, Gaudence Lyimo.
Wanaodaiwa kuuawa siku hiyo kwa kupigwa risasi na polisi wakiwa kwenye
maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha ni Denis Shirima, Omary Ismail na
raia wa Kenya, Paul Juguna.
Awali kabla ya mkutano huo wa jana kuanza majira ya saa nne asubuhi,
viongozi wa CHADEMA wilaya na mkoa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini,
Godbless Lema walitembelea vituo mbalimbali vya yatima na kutoa msaada
wa mchele kilo 20 na mafuta ya kula lita tano kwa kila kituo.
Katibu wa CHADEMA wilayani hapa, Martin Sarungi alisema wamepanga
kuendelea na kazi hiyo hadi Januari 21 ambapo kwa siku ya jana
walifanikiwa kutembelea kituo cha Huruma Group kilichopo Kata ya
Ngarenaro kinachohudumia waathirika wa virusi vya ukimwi, kituo cha
watoto yatima cha Ansaar Muslim Youth Center kilichopo Kata ya Sombetini
kinachohudumia watoto wa kike zaidi ya 30, kituo cha watoto yatima cha
Kibowa kilichopo Kata ya Lemara na kile cha Karama kilichopo Kata ya
Olorien.
Sarungi alisema kuwa katika kipindi hicho wanatarajia kutembelea jumla
ya vituo vya watoto yatima 12, wafungwa na mahabusu kwenye gereza kuu
la mkoa la Kisongo na wagonjwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru
kwa lengo la kuwasaidia, kuwafariji na kuwatia moyo.
Kwa upande wake diwani wa viti maalum, Viola Likindikikoki (CHADEMA)
alisema kuwa yeye na madiwani wenzake wataendelea na msimamo wa
kutomtambua meya kwani licha ya kuingia kwenye wadhifa huo kinyume na
sheria, pia kiti anachokalia kinanuka damu ya wananchi watatu wa Jiji la
Arusha waliouawa bila sababu.
Naye kiongozi wa madiwani wa CHADEMA kwenye Halmashauri ya Jiji la
Arusha, Isaya Doita aliwataka wananchi wa jiji hilo kuhakikisha
wanashiriki kwenye vikao vya shule wanazosoma watoto wao ili waweze
kuzibana bodi za shule na walimu wakuu juu ya michango mbalimbali
wanayokusanya, lakini haina tija.
No comments:
Post a Comment