BAADA ya kuwa nje ya Bunge kwa takriban miezi tisa baada ya
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kumvua ubunge Aprili 4 mwaka jana, Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), ameingia ofisini kwake rasmi
huku akiwa na mikakati mipya ya kuendelea kumpinga meya wa jiji hilo,
Gaudence Lyimo.
Lema ambaye alirejeshewa ubunge wake na Mahakama ya Rufaa Tanzania
Desemba 22, mwaka jana, amewataka pia Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John
Mongela, na Mkuu wa Mkoa huo, Magessa Mulongo, kuacha kutoa matamko ya
kisiasa yenye kulenga kukipiga vita chama chake cha CHADEMA.
Alisema kuwa badala yake wajikite kwenye kusimamia shughuli za
maendeleo ya wananchi kama Katiba ya nchi inavyowaelekeza na waelewe
kuwa wabunge na madiwani toka vyama vyote wana hadhi sawa kwani ni
wawakilishi wa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Lema aliahidi
kuendelea kupinga unyanyasaji unaofanywa kwa wafanyabiashara wadogo
maarufu kama Wamachinga ambao alidai kuwa idadi yao imekuwa ikiongezeka
kila kukicha.
Alisema kuwa hali hiyo imetokana na serikali kushindwa kuzalisha ajira
kupitia viwanda na mashamba huku ikishindwa kutoa elimu ya ujasiriamali
hatua aliyodai inaongeza idadi ya Machinga hao ambao wanatafuta fedha
za kujikimu.
Lema ambaye alisindikizwa na kundi kubwa la wananchi wa jiji la Arusha
wakiwemo viongozi mbalimbali na madiwani wa CHADEMA toka halmashauri
hiyo, aliweka bayana kuwa msimamo wake wa kuendelea kutomtambua Meya
Lyimo bado uko palepale.
Alifafanua kuwa sasa amekuja na staili mpya ya kumpinga kwa hoja
kwenye vikao anavyoviongoza badala ya kutoka nje kama walivyokuwa
wakifanya na madiwani wake.
“Nitashiriki kwenye vikao vya halmashauri endapo kikao cha kamati kuu
ya CHADEMA kitakachokaa mwezi huu kitaturuhusu mimi na madiwani
wenzangu. Ingawa tuko wachache baada ya kuwatimua wengine lakini
tunataka ufanyike uchaguzi halali wa Meya,” alisema.
Alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na viongozi wote wa serikali
wilaya na mkoa isipokuwa hataki kuona uonevu kwa kina mama wauza mboga
sokoni wakipigwa viboko na mgambo ukiendelea.
Lema aliongeza kuwa neno ‘Machinga’ limekuwa likitumika kuwanyanyasa
wafanyabiashara wadogo ambao wengi ni chini ya umri wa miaka 18 ambao
alidai wanatokana na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari.
Aliwataka viongozi hao wa mkoa kumshauri Rais Jakaya Kikwete kufuta
hati ya kiwanja kilichokuwa eneo la wazi la Kilombero lililouzwa
kifisadi na kulirudisha kwa wananchi ili liweze kutumika na Machinga
hao.
Katika hatua nyingine, Lema aliitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza
uchaguzi mdogo kwa kata tano za Kimandolu, Sombetini, Themi, Erelai na
Kaloleni ambazo zimekuwa wazi kwa kipindi kirefu baada ya madiwani wake
kuvuliwa uanachama na CHADEMA na yule wa Sombetini kujitoa CCM.
Alisema kuwa CHADEMA itaadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya vifo
vya watu watatu walioaga dunia wakati wa maandamano yao ya Januari 5 ,
2011 kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Ngarenaro.
No comments:
Post a Comment