MKUU wa Mkoa (RC) wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Masawe,
amekemea vitendo vya askari polisi kutumia nguvu kubwa katika
kukabiliana na raia wema pamoja na kuwanyima haki zao.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa kauli hiyo ofisini jana alipozungumza na
waandishi wa habari alipokuwa akitoa salamu za mwaka mpya 2013 kwa
wananchi wa mkoa huo.
Alisema wananchi wamekosa imani na serikali kutokana na baadhi ya
watendaji wake na walioko katika kutumikia vyombo vya dola kukiuka
maadili ya utumishi na kusababisha uvunjifu wa amani.
Aliwasihi wakuu wa wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na
usalama kufanya kazi karibu na wananchi na kusikiliza kero zao kisha
kutafuta ufumbuzi, ili wapate haki zao ikiwa ni pamoja na kupata huduma
za kijamii.
“Kitendo cha kukiuka miiko ya kazi kwa watumishi wa vyombo vya dola na
kuvunja sheria kimewafanya wananchi kujichukulia sheria mikononi na
kusababisha uvunjifu wa amani katika maeneo yao na hii ni hatari kwa
usalama wa taifa,” alisema Kanali Masawe.
Kutokana na hali hiyo, Masawe aliahidi kufa na kupona na watumishi
wote watakaobainika kuwanyanyasa wananchi kwa kukiuka maadili ya kazi
katika mkoa huo na kwamba wananchi wanatakiwa kuishi kwa amani, ili iwe
rahisi kwao kujiletea maendeleo.
Aidha, aliwashauri wananchi kuepuka vitendo vya kulipa visasi na
kujengeana chuki pamoja na imani za kishirikina na badala yake
waoneshe upendo, mshikamano na ushirikiano kwa watendaji waadilifu, ili
kulinda usalama wao na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, aliwaagiza wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na
Idara ya Uhamiaji kuhakikisha wahamiaji haramu walioko katika wilaya zao
wanaondoka kabla ya msako utakaojumuisha kuondoa mifugo haramu iliyoko
ndani ya mapori ya hifadhi ndani ya mkoa huo haujaanza.
No comments:
Post a Comment