MBUNGE wa Mpanda Mjini, Said Arfi (CHADEMA) amewashambulia
mawaziri wa Wizara ya Uchukuzi kwa madai kuwa wanatoa majibu ambayo
hayakidhi viwango.
Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akiuliza maswali ya nyongeza
kwa kuitaka serikali itoe majibu ya kuwaeleza Watanzania hususani wa
Mpanda ni kwanini stesheni ya eneo hilo haina nyumba ya kusubiria gari
moshi (treni) wala choo.
Mbunge huyo pia aliitaka serikali ieleze ni lini safari za garimoshi
zitaanza kutolewa kila siku ili wananchi waepukane na usumbufu wa
kuuziwa tiketi kwa kulanguliwa.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Sabrina Sungura (CHADEMA) alitaka
serikali kutoa kauli bungeni ni lini itajenga jengo la stesheni ya reli
Kigoma kutokana na jengo hilo kuwa katika hali mbaya na linaweza
kuanguka muda wowote.
Mbunge huyo alisema kuwa licha ya kuwa Kigoma ni sehemu ya kihistoria
kwa kutumia stesheni hiyo, lakini cha ajabu jengo hilo linavuja.
Awali katika swali la msingi, Arfi alitaka kujua ni lini serikali
itajenga jengo la Shirika la Reli lenye hadhi katika stesheni ya reli
Mpanda.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, alisema
serikali ina nia njema ya kuboresha miundombinu ya shirika hilo yakiwemo
majengo ya stesheni zote nchini.
Tizeba, alisema kuwa, kwa sasa serikali inatafuta fedha ili
kuhakikisha wanajenga kituo cha stesheni ya Kigoma ili kuendelea
kukifanya kuwa cha kihistoria.
No comments:
Post a Comment