MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, Mganda, Emannuel Okwi,
huenda akaadhibiwa na klabu yake ya
Simba kwa kushindwa kujiunga kwa wakati na wenzake walioko Zanzibar
wakishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi litakalofikia kilele Januari
12.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema jijini Dar es Salaam
jana kuwa, Okwi alitakiwa kuwasili nchini na kujiunga na kambi Januari
2, lakini ameshindwa kufanya hivyo bila ya kutoa taarifa kwa uongozi.
Mtawala alisema, kutokana na nyota huyo kushindwa kufika nchini kwa
muda muafaka sambamba na kugoma kupokea simu anapopigiwa, uongozi
umeamua suala hilo kulipeleka katika benchi la ufundi, ambalo
litapendekeza hatua ya kuchukuliwa nyota huyo.
Aidha, Mtawala alifafanua kuwa, uamuzi huo sio kwa mchezaji huyo
pekee, bali yeyote anayefanya vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu
atakutana na rungu la utawala.
"Sisi kama uongozi tumemuachia Meneja, Moses Bassena na tunaamini
atakuwa makini katika suala hili, hivyo Okwi atatakiwa kutoa sababu
zinazofanya ashindwe kupokea simu na zinazofanya asije kambini, huku
akijua Ligi inakaribia kuanza na timu iko katika michuano ya Mapinduzi,"
alisema Mtawala.
Katika hatua nyingine, Mtawala alisema, kwa kuwa timu
yao inashiriki michuano ya Mapinduzi, kuna uwezekano
wa kikosi chao kikaondoka nchini kwenda kujinoa nchini Oman Januari
13, siku moja baada ya kumalizika kwa mashindano hayo endapo timu
itakuwa imeingia fainali.
Kuhusiana na kibali cha kocha wao mpya, Mfaransa Patrick Liewig,
alisema kuna uwezekano wa kupatikana Jumatatu au Jumanne ijayo kama
mambo yatakwenda vizuri.
No comments:
Post a Comment