JESHI la Polisi nchini limewataka waathirika wa dawa za kulevya
kushirikiana na jeshi hilo ili kuweza kuwafichua wale wote
wanaoziingiza nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema katika Kituo cha PILIMASSANA ambacho kinahudumia waathirika wa dawa za kulevya jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema kuwa sio dhamira ya jeshi hilo kuwaona waathirika hao wakipelekwa gerezani kwa wizi wa vitu vidogo vidogo vikiwemo vijiko na sahani.
Kamanda Kiondo alisema kuwa, jamii itaona fahari iwapo kutakuwa na
ushirikiano wa pamoja na kuwafichua wauzaji wa dawa hizo ili kuweza
kukabiliana nao.
“Nia yetu ni kuwaona mnarudi na kuwa mabalozi wazuri, hatuna haja ya
kuwapeleka jela ila tunachohitaji ni kusaidia ili kujua wanaoingiza
dawa hizo na kuweza kuchukuliwa hatua,” alisema.
Alisema kuwa vijana hao sio wahalifu bali matumizi ya dawa za kulevya
ndiyo yanayosababisha kufanya vitu ambavyo havikubaliki ndani ya
jamii.
Naye Mkurugenzi wa PILIMASSANA Foundation, Pili Massana, alisema kuwa
dawa za kulevya ni janga la kitaifa, hivyo ameiomba jamii kuacha
kuwanyanyapaa waathirika na badala yake washirikiane ili kutatua tatizo
hilo.
“Kituo hiki kilianzishwa Aprili mwaka jana ambapo mlezi wetu ni
Zacharia Hanspope, kilianza na waathirika 17, hadi sasa tumeweza
kuwasaidia waathirika zaidi ya 80 ambao wanaendelea na shughuli za
ujenzi wa taifa huko uraiani,” alisema.
Alisema kuwa wamekuwa wakipata vijana wengi wanaofika na kuhitaji
kupewa msaada kituoni hapo, lakini kutokana na uhaba wa kifedha
wanashindwa kupokea waathirika wengi
No comments:
Post a Comment