WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaponda
watu wanaoipinga tume aliyoiunda kuchunguza sababu za idadi kubwa ya
wanafunzi wa kidato cha nne kuvurunda katika mtihani huo akieleza kuwa
huenda watu hao hawaelewi ukubwa wa tatizo na jinsi linavyotakiwa
lishughulikiwe. Katika matokeo hayo ambayo yanatajwa kuwa mabovu kuliko
yoyote yaliyowahi kutokea katika historia ya Tanzania, asilimia 60 ya
wanafunzi waliofanya mtihani huo walipata sifuri.
Pinda alisema hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa siku moja kuhusu mafanikio ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Alisema ni lazima waelewe kuwa mambo yatakayoangaliwa ndani ya uchunguzi huo ni mengi na si kama wanavyofikiri baadhi ya wanaopinga hivyo ni muhimu wakatulia na kusubiri matokeo.
“Wengine wanasema tume zipo nyingi, si kweli kwamba zipo nyingi na hazifanyi kazi, kila mtu ana mawazo yake, jambo hili ni kubwa na lazima lishughulikiwe kwa ukubwa wake,”alisema Pinda.
Pinda alisema hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kukamilisha tume hiyo na itaanza kazi kati ya leo au kesho.
“Tuko katika hatua za mwisho kwa kuwa tulihitaji kuhusisha wadau wote ikiwa ni pamoja na Zanzibar, dini mbalimbali, sekta binafsi pamoja na wabunge kadhaa ili tuunganishe nguvu na leo au kesho itaanza kazi rasmi,”alisema Pinda.
Wiki iliyopita Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo alisema kuwa tume hiyo inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote wiki hii, ambapo itajumuisha Chama cha Wamiliki wa Shule ya Sekondari na Vyuo Binafsi.
Lyimo aliwataja wadau wengine watakaohusika katika uchunguzi huo kuwa ni kutoka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa)
“Tume hiyo itahusisha asasi zisizo za kiserikali (NGOs), zinazojishughulisha na masuala ya elimu. Wazazi, walezi na wananchi wote kwa jumla watoe ushirikiano kwa tume, ili ifanye kazi kwa ufanisi,” alisema Lyimo.
No comments:
Post a Comment