KESI ya kukashifu, iliyokuwa ikilikabili gazeti la MwanaHALISI, imetupiliwa mbali na mdai ametakiwa kulipa gharama zote za kesi.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam,
Warialwande Lema, katika hukumu yake Jumatano, alisema ili maneno yawe,
au yaonekane kuwa ya kashfa, sharti yawe ama si ya kweli au yawe ya
uongo.
Alisema kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakama haikuona chochote kile kilichothibitisha madai ya kashfa.
Juma Jaffari Nyaigesha, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msewe,
jijini Dar es Salaam ndiye alilishtaki gazeti akidai kuwa kwa habari na
makala zilizochapishwa katika matoleo yake matano, alikashifiwa na
kuvunjiwa heshima mbele ya jamii.
Mdai alimshtaki mhariri wa gazeti, Jabir Idrisa, mshauri wa gazeti,
Ndimara Tegambwage, Stella Kajuna – mkazi wa Msewe, mhariri mkuu,
kampuni inayochapisha gazeti, Hali Halisi Publishers Limited, kampuni ya
uchapaji ya Printech na kampuni nyingine ya uchapaji, Tanzania Standard
Printers Limited.
Nyaigesha alidai kuwa matoleo matano ya MwanaHALISI yalikuwa na taarifa zilizomkashifu na kumwondolea hadhi mbele ya jamii.
Aliyataja matoleo hayo kuwa yale ya 10, 12, 24, 31 Oktoba 2007 na 14 Oktoba 2008.
Katika matoleo hayo kulikuwa na habari na makala juu ya madai ya
kuwepo vitendo vya uhalifu Msewe, ukosefu wa amani na matumizi mabaya ya
madaraka ambavyo Nyaigesha alidai vilikuwa vinaelekezwa kwake.
Katika hukumu yake, hakimu Lema alisema kwanza mdai hakuleta hata
shahidi mmoja kuthibitisha madai yake na kwamba yeye mwenyewe hakuweza
kuthibitisha kuwa amekashifiwa.
Hata takwimu za kura za uchaguzi alizopeleka mahakamani, zilionyesha
kuwa hata baada ya kuandika yaliyokuwa yakitokea Msewe, katika uchaguzi
uliofuata alipata kura nyingi, jambo ambalo lilikinzana na madai ya
kukashfiwa.
Hakimu alisema Jaffari ni kiongozi na kile walichofanya waandishi
kilikuwa ni mjalizo halali na wa haki juu ya kiongozi na uongozi wa umma
na siyo kashfa.
Alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na walalamikiwa, ushahidi wa
maandishi kutoka kwenye kata na hata kauli ya mdai kuwa mmoja wa
walalamikiwa alipigwa na kwamba yote hayo yalidhihirisha umuhimu wa
kilichoandikwa.
MwanaHALISI ilikuwa ikitetewa na wakili maarufu, Mabere Marando,
wakati Tanzania Standard Printers Ltd, iliwakilishwa na wakili Audax
Kahendaguza Vedasto wote wa Dar es Salaam.
Kuhusu wachapaji wa gazeti, hakimu alisema hawakuwa na hatia kwa kuwa
hawakutenda kashfa yoyote, kwa vile hakuna kashfa iliyothibitishwa.
Aidha hakimu alikubaliana na hoja kwamba mchapaji anayefanya kazi
aliyopewa na kuirejesha kwa mhusika, hawezi kuwa ametenda kashfa.
Alipoulizwa Mkurugenzi Mtendaji wa HaliHalisi Publishers, Saeed
Kubenea, juu ya hatua anayojiandaa kuchukua, alisema hajakaa na wakili
wake kupanga hatua inayofuata.
No comments:
Post a Comment