SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limewasilisha rasmi ombi la
kukutana na serikali kuhusu msigano uliopo baina ya pande hizo mbili,
lakini wakitoa sharti kuwa hawako tayari kuketi na Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.
Akizungumza kwa kujiamini, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Angetile
Osiah, alisema jana kwamba hawataki kujadili suala hilo na Makalla kwa
sababu ameonekana wazi kuwa na upande kupitia kauli zake mbalimbali.

Alisema kabla na baada ya serikali kutangaza kuifuta katiba mpya ya
TFF ya mwaka 2012 na kuitambua ya mwaka 2006, Makalla amekuwa akitoa
kauli zinazoashiria wazi kuwa upande mmoja wa wagombea walioenguliwa na
Kamati ya Rufaa.
Osiah alisema kwa mazingira hayo, wao TFF hawataketi na Makalla
kujadili jambo hilo kwa maslahi ya soka nchini kwa sababu kupitia vyombo
vya habari hasa radio, amekuwa akilishutumu shirikisho hilo tangu
Kamati ya Rufaa iwaengue baadhi ya wagombea.
“Hata kama waziri asipokuwepo, hatuko tayari kufanya mazungumzo yoyote
na naibu wake, tunasema hivyo kwa sababu tayari Makalla (Amos),
ameonyesha yeye ni mdau wa upande fulani, hatuna imani naye,” alisema
Osiah na kuongeza:
“Kwanza alianza kuongelea ishu hii mara baada ya Kamati ya Rufaa
kuwaengua baadhi ya wagombea, yeye akiwa nyumbani kwake akatoa tamko,
halafu pili akiwa Morogoro mjini, aliitisha mkutano na waandishi wa
habari juu ya msimamo wake kuhusu mchakato wa uchaguzi na mabadiliko ya
katiba,” alisisitiza Osiah.
Osiah alisema Makalla kama kiongozi mwenye dhamana ya michezo,
hakupaswa kuonyesha kuwa upande gani kabla ya kutoa nafasi na kusikiliza
pande zote mbili kwa maana ya walalamikaji na walalamikiwa.
Aliongeza kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro uliopo ni wao TFF kuonana
na Mukangara na sio Makalla ambaye anaonekana wazi ni sehemu ya tatizo
akiwa upande wa mdau aliyeenguliwa.
Hata baada ya Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga, kutoa msimamo kuwa
uamuzi wa serikali wa kuibatilisha katiba ya 2012 na kuitambua ya mwaka
2006, hautekelezeki, hivyo wanataka kukutana na waziri, Makalla alisema
milango iko wazi, lakini TFF ijue uamuzi wa awali wa serikali
hautabadilika.
Kuhusu ombi la kutaka kuonana na serikali, Osiah alisema
waliliwasilisha wizarani tangu Machi 4, ikipendekeza kikao hicho
kifanyike Machi 7 au 13 kwani viongozi wa juu wa shirikisho hilo
watakuwa kwenye mkutano nchini Morocco.
Uamuzi wa TFF kukutana na serikali ulifikiwa na Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho hilo iliyoketi Machi 2, kujadili tamko ya Waziri Mukangara
kutengua matumizi ya katiba hiyo mpya kwa hoja kwamba ilipitishwa
kinyume cha sheria ya michezo ya mwaka 1967 na marekebisho yake 1971.
Tanzania Daima ilipomtafuta Makalla jana jioni kwa njia ya simu kuhusu
sharti la TFF, alisema TFF hawana ujanja kwa hilo kwani yeye ndiye
watakutana naye kutokana na kitengo cha michezo kuwa chini yake.
Makalla alisema kwa siku zilizopendekezwa, Mukangara atakuwa safarini
nje ya nchi kwa siku 10 na kusema anashindwa kuelewa msimamo wa
shirikisho hilo kwani awali walitaka kukutana na waziri, sasa wanatoa
sharti juu ya nani wakutane naye.
No comments:
Post a Comment