MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, (CHADEMA), amewataka
Watanzania watarajie mapanbano makubwa zaidi bungeni, hata ikibidi
ngumi kupigwa, ili kuleta ustaarabu na kutetea haki ya kidemokrasia
katika chombo hicho cha kutunga sheria.
Ndesamburo ambaye amekuwa bungeni tangu mwaka 2000, alisema hayo jana
katika mahojiano mafupi na gazeti hili, ofisini kwake Moshi Mjini.
Alisema nyakati zimebadilika na wabunge wa mwaka 2013 si sawa na wa
mwaka 2000; kwani hawa wa sasa hawako tayari kuona kanuni zinavunjwa
waziwazi.
Ndesamburo alikuwa akizungumzia kauli ya Spika wa Bunge, Anna Makinda,
na Naibu wake, Job Ndugai, ambao wanadai kuwa baadhi ya wabunge wa
CHADEMA ni vinara wa fujo bungeni.
Alisema siasa za sasa ni za vijana, si za wazee kama ilivyokuwa huko
nyuma na kwamba wazee wanapaswa kuelewa kuwa nyakati zimebadilika.
Alisema kwamba katika siasa za kuelekea mwaka 2015, CHADEMA ina nafasi
kubwa ya kushinda ili kuwaletea Watanzania maendeleo waliyokosa kwa
miaka zaidi ya 50.
Alisema: “Lazima tujifunze kubadilika, hizi ndizo siasa za wakati
huu. Watu wasidhani vijana hawa wa CHADEMA, hata vijana wa CCM… maana
yake kitu kimoja ambacho nimekiona, kama tunajaribu kufikiria sasa, watu
wasidhani ni CHADEMA… lakini kule ndani mpaka vijana wa CCM wanafanya
vurugu. Ukitazama ile filamu iliyoletwa na TBC ilionyesha CHADEMA tu
haikuonyesha upande wa CCM walioshangilia, haikuonesha kabisa; jambo
ambalo si sahihi.
“Kwa hiyo watu wajifunze kwenda na wakati. Zamani Bunge lilikuwa
limetawaliwa na wazee. Sasa kuna vijana. Vijana ni tofauti na wazee.
Lazima wazee waanze kujua vijana wanataka nini. Sheria na kanuni
zinazoendesha Bunge, vijana wanazijua, zinapovunjwa ni rahisi kuelewa.
Zamani hakuna aliyekuwa anajali hilo.
“Hizi fujo ni demokrasia. Bunge linashika hamasa, limekuwa zuri. Wala
wasione haya. Hii ni mwanzo tu, tutaona mengi hata ngumi zitapigwa mle
ndani. Ndiyo ustaarabu, hilo ndilo Bunge. Unaponyimwa haki yako,
unataka mtu afanyeje?”
Katika Bunge la Februari, Bunge lilitawaliwa na fujo, baada ya Spika
wa Bunge, Anna Makinda, na Naibu Spika, Job Ndugai, kuliendesha Bunge
kinyume cha kanuni na kusababisha kuzomewa na wabunge wa upinzani
waliodai Spika na naibu wake wanapinda kanuni.
Mjadala mkali ulianza wakati wa kujadili hoja binafsi za mbunge wa
Ubungo, John Mnyika, mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, na
Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia. Uongozi wa Bunge uliahirisha
shughuli za Bunge mara kadhaa baada ya hali ya kutoelewana na ubishi
mkali kutokea ndani ya Bunge.
Akizungumzia hali hiyo, Makinda alinukuliwa akisema, “Hata hivyo,
imelazimu kuahirisha mijadala ya hoja binafsi kutokana na tabia
iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge na hivyo kuamua
kwa makusudi kuanzisha vurugu na hivyo kulifanya Bunge lianze kupoteza
heshima yake ya kibunge.”
Alisema hoja binafsi za wabunge zinaongozwa na kanuni za Bunge kuanzia
kanuni ya 53 hadi 58, na kanuni za majadiliano zinaongozwa na kanuni
kuanzia 59 hadi 71 ambazo kwa ujumla wake zikifuatwa kama inavyotakiwa
vurugu haiwezi kutokea bungeni.
Makinda ambaye alionekana kuzungumza kwa jazba, alisema katika mkutano
huu imeonyesha waziwazi baadhi ya wabunge kwa makusudi na kwa nia ya
kupotosha wananchi wanatumia vibaya kanuni hizo na wakati mwingine
kuwadanganya wananchi ambao kwa bahati mbaya kanuni hizi hawazifahamu.
Ubabe huo wa Spika na naibu wake ulisababisha kwa mara ya kwanza tangu
kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2010, wabunge wa vyama vya upinzani
kuungana kumsusa Spika na Naibu Spika, wakipinga hatua yake ya
kupindisha hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wabunge wa upinzani.
Wabunge wa vyama vya upinzani waliotoka kupinga ubabe wa Spika
kinyume cha kanuni ni wa vyama vya CHADEMA, CUF, UDP, TLP na
NCCR-Mageuzi ambao waliungana kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, kupinga
hatua ya Ndugai kuwaburuza katika kupitisha hoja ya Mbatia.
Hoja hiyo binafsi iliyoainisha udhaifu katika mfumo wa elimu nchini,
iliwasilishwa na kuibua mjadala mzito bungeni, huku kambi ya upinzani
ikikubali hoja ya Mbatia kutaka kuunda kamati teule wakati wabunge wa
CCM wakipinga, hoja iliyosababisha hadi sasa Wazairi Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuunda tume inayotafuja tatizo la kufeli kwa
wanafunzi wa mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment