MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), amemuonya mkuu
wa mkoa huo, Magesa Mulongo, kuacha kutumia nguvu kubwa kudhibiti
harakati za chama, vinginevyo atashindwa kufanya kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Lema alimtaka mkuu
huyo kuacha kuingilia majukumu ambayo si yake na kwamba endapo
ataendelea wataitisha mikutano na kuwasihi wananchi
kutompa ushirikiano.
Kauli ya CHADEMA ilikuja baada ya mkuu wa mkoa kusikika katika vituo
vya radio vya mjini Arusha jana asubuhi akiwataka vijana kutoshiriki
maandamano ya chama hicho akidai viongozi wao wasingelidhurika na
matokeo ya maandamano hayo.
CHADEMA jana iliahirisha maandamano yake yaliyokuwa yafanyike katika
majiji manne likiwemo la Arusha ili kumshinikiza waziri wa elimu na
naibu wake kuachia ngazi kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne
2012.
Mulongo katika kujaribu kufifisha nguvu ya CHADEMA, alitumia vituo
hivyo vya redio akisema, “Vijana mnahamasishwa kuandamana, wakati
mnafanya hivyo viongozi wa chama watakuwa baa wakinywa bia nyie
mnakabiliana na vyombo vya dola, hivyo nawaonya kutojiunga katika
maandamano hayo.’’
Kufuatia kauli hiyo, Lema alisema ameshangazwa na mkuu huyo wa mkoa
kwani suala la maandamano lilikwishatolewa tamko na viongozi wa makao
makuu wa chama hicho baada ya kushauriana na Mkuu wa Jeshi la Polisi
Nchini (IGP), Saidi Mwema.
“Sasa hivi hakuna mawasiliano ndani ya serikali kwani suala la
maandamano lilishamalizwa na viongozi wa kitaifa yeye bado analiendeleza
na kukashifu chama, tutamfanya akose ushirikiano katika kazi zake
akiendelea na tabia hii,’’ alisema Lema.
Naye Mwenyekiti wa Vijana wa Mkoa wa chama hicho, Ephata Nanyaro, amempa siku tatu Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Gilles
Bilabaye, akimtaka kukiomba radhi chama hicho na wananchi wa Arusha kuwa wanataka kuandamana kwa sababu ni walevi.
“Huyu OCD anatuambia sisi ni walevi wa viroba pamoja na wananchi ndio
maana tunaandamana! Tunaomba ndani ya siku tatu atuombe radhi kabla
hatujaamua kutumia nguvu ya umma kushughulika naye!’’ alisema Nanyaro
ambaye ni Diwani wa Kata ya Levolosi.
Juzi OCD huyo alinukuriwa katika maeneo mbalimbali ya mjini Arusha
alikokuwa akizunguka na kipaza sauti akiwa ndani ya gari namba PT 1844,
akiwazuia wananchi kutojitokeza katika maandamano hayo.
Alipotafutwa na gazeti hili kufafanua madai ya kutumia nguvu kubwa
katika kukidhibiti chama hicho, Mulongo alijibu kwa kifupi kuwa
anawatakia kila la kheri kwa wanachotaka kukifanya.
“We ni mwanahabari nadhani unatambua mimi ni nani katika mkoa huu,
basi kama ni hivyo nawatakia kila la kheri,’’alisema Mulongo.
OCD yeye alikataa kuzungumzia shinikizo hilo la CHADEMA akisema
aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa, Loberatus Sabas, lakini naye alidai
kutosikia kauli za OCD wake.
No comments:
Post a Comment