Dar es Salaam. Rais Xi Jinping wa China ameahidi kuendelea
kuipiga jeki Afrika ili kukabiliana na changamoto za kimaendeleo, huku
akisema kuwa suala la utoaji misaada yenye masharti magumu siyo ajenda
ya Serikali yake.
Jinping akitumia jukwaa la Tanzania
kutambulisha sera yake kwa nchi za Afrika alisema kwamba bara hilo
limepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwamba nchi yake itaimarisha
uhusiano uliopo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Alisisitiza kwamba ushirikiano wenye tija ni ule unaozingatia “majadiliano na maridhiano” na kwamba Serikali yake imetenga kiasi cha Dola za Marekani 20 bilioni kufadhilia miradi mbalimbali ya maendeleo Afrika.
“China haitakuwa tayari kutoa masharti kwa taifa lolote… Tunataka kutoa fursa zinazofanana,” alisema Rais, ambaye alishika rasmi wadhifa huo Machi 14, mwaka huu.
Alisema China haitaingilia masuala ya ndani ya nchi, huku akisisitiza kwamba shabaha ya nchi yake ni kuendelea kupalilia ushirikiano mwema uliodumu kwa miongo kadhaa na siyo kujihusisha na migogoro.
Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanadai kuwa, kauli ya kiongozi hiyo ni kama ujumbe wa onyo kwa baadhi ya nchi za Magharibi ambazo zinalalamikiwa kuendesha sera zinazominya ustawi wa Afrika.
Mhadhiri katika Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR), Dk Ahmed Mtengwa alisema: “Ni hotuba inayofungua njia kwa Afrika..., amezungumzia ushirikiano unaolingana yaani `win win situation’ (kila upande ufaidike), hivyo kwangu ninayaona matumaini.”
Rais Jinping, aliyekuwa katika ziara ya siku mbili nchini na juzi usiku alisaini mikataba 17 inayohusu sekta za kilimo, afya na miundombinu.
Mkataba wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani ni kati ya miradi mikubwa iliyomo kwenye makubaliano hayo na ujenzi wake utafanywa na Kampuni ya Merchants Holding ya China na utakwenda sanjari na ujenzi wa barabara inayounganisha bandari hiyo.
Pia katika bandari hiyo itaunganishwa na Reli ya Kati na na ile ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ili kurahisisha usafiri wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Mikataba mingine itahusiana na uboreshaji wa sekta ya viwanda, kilimo hasa kile cha tumbaku ikiwamo kuwatafutia soko wakulima kutoka Mikoa ya Tabora na Ruvuma ili waweze kuuza zao hilo katika soko la China pamoja na kulipatia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zana za kufanyia kazi.
Rais huyo, ambaye Tanzania ndiyo nchi ya kwanza barani Afrika kuitembelea, alizindua na kukabidhi rasmi Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere kilichoko jijini Dar es Salaam ambalo ni jengo la ghorofa tatu na lenye kumbi nne za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 1,800 kwa wakati mmoja.
Ujenzi wa kituo hicho uligharimu Dola za Marekani 29.7 milioni zilizotolewa na Serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Rais huyo alisifu ushirikiano wa muda mrefu baina ya taifa lake na Tanzania na kusisitiza kuwa nchi hizo zitaendelea kusaidiana kama sehemu ya kuenzi misingi iliyowekwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Tung.
Rais Jinping aliondoka jana jioni kwenda Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi ikiwamo Brazil, Urusi, India, China na Afrika ya Kusini (BRICS).
No comments:
Post a Comment