Timu
ya uchunguzi wa matukio ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha
(IFM) waliodai kufanyiwa vitendo vya ulawiti wakati wakiwa hosteli ya
Kigamboni, imetoa matokeo ya ripoti yake jana na kubaini kuwa madai ya
wanafunzi hao hayakuwa ya kweli.
Timu hiyo iliundwa baada ya wanafunzi wa
chuo hicho kufanya maandamano Januari 14, mwaka huu kuelekea makao makuu
ya jeshi la polisi nchini kupeleka malalamiko yao dhidi ya uhalifu na
ulawiti uliokithiri maeneo yao.
Kufuatia maandamano hayo ambayo
yalitulizwa kwa mabomu ya machozi, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliunda timu ili kuchunguza madai ya
wanafunzi hao.
Timu hiyo ilihusisha wapelelezi kutoka Polisi Kati, Temeke, Kigamboni, wanafunzi wanne, watendaji wa kata na wadau wengine.
Akitoa taarifa ya timu hiyo jana jijini
Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo,
alisema imebaini hakuna hosteli katika maeneo wanaoishi wanafunzi hao
bali wanaishi nyumba za kawaida zenye wapangaji wengine.
Kamanda Kiondo alisema licha ya juhudi
zilizofanywa na timu hiyo lakini hawajapokea taarifa zozote za
kulawitiwa kwa wanafunzi hao.
Alisema katika suala hilo, timu
ililazimika kutumia dawati la jinsia kama sehemu ya kupata taarifa za
wanafunzi waliodai kufanyiwa vitendo vya kulawitiwa lakini hakuna
aliyeripoti.
"Tunaamini suala hili lilipewa kipaumbele
wakati wa maandamano ili kuleta mvuto na hamasa kwa jamii ili
kuyafanikisha maandamano hayo," alisema.
Akifafanua kuhusu nyumba ambazo wanafunzi
hao wamepanga, Kiondo alisema hazina usalama kwao na kwamba sio hosteli
kama walivyokuwa wakiziita.
"Sehemu walizopanga ni makazi ya watu
wengi, na sio nyumba moja ambayo imepangisha wanafunzi wa IFM bali
wamechanganyika na wananchi, kwa hiyo ulinzi haupo," alisema.
Alisema kutokana na hilo vitendo vya wizi
wa mali mbalimbali ambazo wanafunzi waliviripoti vimekuwa vikiitokea
katika jamii nzima na sio wanafunzi peke yao.
Pia alisema timu hiyo imebaini kuwa wenye nyumba hizo hawajachukua hatua za usalama wa wapangaji wao.
Kuhusu kesi ambazo zimeripotiwa polisi,
kamanda alisema mbili kati ya zote ndizo zilizofikishwa mahakamani na
nyingine upepelezi wake umekuwa mgumu kufanyika kutokana na mazingira ya
tukio lenyewe.
Mapendekezo ya nini kifanyike, Kiondo
alisema IFM inapowadahili wanafunzi wake inatakiwa kuwahakikishia
usalama wa mahali wanapoishi (hosteli).
Alisema tayari jeshi la polisi limefanya
kazi ya kuhakikisha ya kutoa elimu kwa wanafunzi hao na jamii
iliyowazunguka kuhusu ulinzi shirikishi na wameipokea.
Alisema wamewashauri wamiliki wa nyumba
hizo kuweka ulinzi kwa sababu jeshi la polisi haliwezi kupeleka ulinzi
kwa sababu kiutaratibu walitakiwa wawe na walinzi wao.
Pia alisema wametoa elimu kwa wanafunzi
kuacha tabia ya kutembea mmoja mmoja badala yake wanapokuwa na mali
watembee kwa vikundi ili usalama uwepo.
Kuhusu timu alisema kazi waliyoifanya itakuwa ni endelevu mpaka hapo chuo hicho kitakapokuwa na hosteli kwa wanafunzi wake.
Timu hizo zilikuwa zikifanyakazi ya kuchunguza madai ya wanafunzi ya kuvamiwa mara kwa mara na kuporwa mali na vibaka.
Nyingine ni madai ya vitendo vya ulawiti
kwa wanafunzi hao ambavyo vilifanywa na vibaka hao na taarifa kuwa jeshi
la polisi limeshindwa kuwachukulia hatua wahalifu hao.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment