Habari na Nipashe
Hospitali
ya Amana, jijini Dar es Salaam, imedaiwa kumtesa mjamzito kwa kumpiga
na kuchelewa kumpa matibabu wakati akiwa katika chumba cha upasuaji.
Akitoa madai hayo, Edna Mjema, (pichani),
aliyekuwa amelazwa katika hospitali hiyo Jumapili iliyopita, alidai
kucheleweshewa matibabu na kupigwa wakati alipopelekwa katika chumba cha
upasuaji.
NIPASHE Jumapili ilipoongea na mgonjwa
huyo anayeishi Chanika, alidai kuwa Machi 16, mwaka huu majira ya saa 7
usiku alikuwa akijisikia vibaya kutokana na hali yake ya ujauzito na
alikwenda hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.
Alisema alikuwa na ujauzito wa miezi sita
na kuwa baada ya kufika hospitalini hapo walimpa dawa na kumtaka arudi
Machi 18 kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha ultra sound.
“Nilipofika nyumbani nilikunywa dawa
nilizopewa ila hali yangu ilizidi kuwa mbaya na ndipo saa 11 ya alfajiri
ilinibidi nirudi hospitalini hapo kwa ajili ya kuwajulisha hali yangu,”
alisema.
Alisema kabla ya kwenda katika hospitali
hiyo, Machi 13, mwaka huu alikuwa akitokwa na maji na kwenda katika
zahanati ambapo alipewa dawa.
Mjema alisema Machi 16, akiwa anamaliza dawa alizopewa alipatwa na maaumivu na kumlazimu kurudi katika kituo cha afya.
Alisema pale alipewa rufaa ya kwenda
hospitali ya Amana na alipofika hospitalini hapo alienda katika wodi ya
wazazi ambapo manesi walimtaka aende wodi namba nne kwa kuwa alikuwa
hajafikia miezi ya kujifungua.
Hata hivyo, alisema alipofika kwenye wodi namba nne hakuna aliyempokea na kuamua kujitafutia kitanda mwenyewe na kulala.
“Nikiwa nimelala kwenye kitanda hicho,
alikuja nesi na kuniondoa na kunieleza kuwa kitanda hicho ni special
(maalumu) kwa watu wanaotoka chumba cha upasuaji, ikanibidi niondoke na
kwenda katika kitanda kingine ambacho kilikuwa kipo wazi,” alisema.
Alisema akiwa kwenye kitanda hicho hakupata huduma yoyote na kila alipowaita wauguzi hakuna aliyemjali.
Mjema alisema hali yake iliendelea kuwa
mbaya hadi saa 9 alasiri aliposhindwa hata kugeuka na kwamba mpaka muda
huo hakuna huduma yoyote aliyoipata.
Alisema ndugu zake walimjulisha ndugu yao
ambaye ni daktari wa Tumbi kuhusu hali ya ndugu yao ya kutopata matibabu
ambaye aliwasiliana na madaktari wa hapo na kuanza kupewa matibabu.
Hata hivyo, alisema daktari baada ya
kufika alimtaka asukume kumtoa mtoto ambapo anadai hakuweza kufanya
hivyo kutokana na kukosa nguvu na ndipo daktari huyo alipokivuta kiumbe
hicho.
Alisema mtoto alitoka akiwa amefariki
lakini kondo lilikuwa limekataa kutoka na ndipo daktari alipomuacha huku
kondo likiwa limebanwa na mkasi.
Alisema wakati anajifungua ilikuwa ni saa 9
mchana na aliendelea kukaa na kondo hilo hadi saa 2 usiku
alipopelekwa chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuondolewa kondo hilo.
Mjema alisema wakati akiwa kwenye chumba
cha upasuaji, daktari aliyemtaja kwa jina moja Dk.Kajura alimtaka aeleze
kama alikuwa ametoa mimba huku akimpiga kwenye tumbo.
“Aliniambia sema ukweli wako kama umetoa
mimba huku akinishindilia ngumi kwenye tumbo kila nikimueleza ukweli
namuona hasira zake anazishushia kwenye tumbo langu. Daktari akasema
kama haujatoa mimba basi utakuwa umeathirika,” alisema Mjema.
Alisema alifanyiwa upasuaji mkubwa kwa
ajili ya kutoa kondo hilo na alielezwa kuwa kondo hilo lilikuwa
limeingia hadi kwenye kizazi na kukipasua kizazi ambapo ilibidi kishonwe
wakati akifanyiwa upasuaji.
Alidai kuwa baada ya kutoka chumba cha upasuaji majira ya saa 6 usiku aliwekewa damu pamoja na maji.
Alisema alipoamka aligundua kuwa damu haisogei na wala maji hayasogei na ndipo alipoomba msaada wa manesi ambao hawakumjali.
Alisema akiwa hospitalini hapo alikuwa na
ndugu yake aliyekwenda kumsaidia na kuona tatizo hilo na kuanza
kumrekebeshia dripu ili damu pamoja na maji ili yaweze kupita.
Alisema wakati ndugu zake wakilalamika
kuhusu hospitali hiyo kuwanyima huduma kwa wakati, waliambiwa kuwa
wanaweza hata wakaenda mahakamani.
“Daktari alituambia kama mnataka muende
mahakamani na wao wana uwezo wa kubadilisha faili la mgonjwa na kuandika
jambo lingine na kwamba wao hawasimami mahakamani kwani wana wakili,”
alisema.
Alisema ndugu zake walikuwa wakilalamika
kutoridhishwa na huduma na baada ya kuwasilisha malalamiko yao ndipo
walipotishiwa kuwa watawafungulia kesi kwa ajili ya kutoa mimba.
Hata hivyo, alisema baada ya kuona hakuna
huduma, ndipo ndugu zake walitaka kumuondoa katika hospitali ya Amana na
kumpeleka katika hospitali nyingine ambapo suala hilo lilizuilika na
kujulishwa kuwa watafunguliwa kesi ya utoaji mimba.
Mjema alisema tangu akiwa na ujauzito wa miezi miwili alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kutokwa na damu ya hedhi.
Mgonjwa huyo ambaye aliruhusiwa kurudi
nyumbani Machi 21, mwaka huu, anaeleza kuwa bado hali yake haipo vizuri
kwani anapata maumivu makali kwenye tumbo.
Mama Mzazi wa mgonjwa huyo, Nafadhai
Kituma alisema ameshangazwa na kitendo cha hospitali hiyo baada ya kutoa
malalamiko yao na kuwabadilikia kwa kumtuhumu binti yake kuwa ametoa
mimba. “Baada ya kulalamika huduma kuwa mbovu, wanatutishia
watatufungulia kesi kuwa mwanangu katoa mimba kwanini tangu mwazo
hawajasema hilo hata sisi hatuogopi kufunguliwa hiyo kesi wale madaktari
wanatuona sisi ni wakuja tunajua haki zetu eti anatueleza wana uwezo wa
kubadilisha kile alichoandika katika faili na kuandika jambo jingine
kwa kuwa wana uwezo huo,” alisema
Kituma alisema mwanae tangu muda mrefu
alikuwa anatamani kupata mtoto kwani mtoto wake wa kwanza kwa sasa ana
miaka 9, sio hospitali ilazimishe kuwa ametoa mimba.
Alisema hawajafurahishwa na vitendo
alivyofanyiwa mtoto wake ikiwamo kupigwa na daktari pamoja na
kucheleweshewa kutolewa kwa kondo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali
ya Amana, Dk. Meshack Shimwela, alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya
tukio hilo alikanusha mgonjwa huyo kupigwa.
Alisema kile walichokiona ndani ya
upasuaji na kile alichokieleza ni tofauti na kwamba hospitali yake
imefanya jitihada kubwa kuokoa hali ya mgonjwa huyo.
“Akithibitisha kwa maandishi nitakueleza
kile ambacho tumekiona kwani kuna miiko ya kazi ambayo hainiruhusu
kuzungumzia labda mgonjwa mwenyewe akubali,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment