PAMOJA na vyombo vya dola kupiga chenga katika kuwakamata
watuhumiwa wa matukio ya kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka na Mhariri Mtendaji wa New
Habari (2006), Absalom Kibanda, serikali imetakiwa iwataje wahusika na
kuwachukulia hatua.
Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya maofisa wastaafu katika vyombo
mbalimbali vya dola, waliozungumza wakidai kwa sasa
vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kwa shinikizo la kisiasa.
Maofisa hao ambao waliomba kuhifadhiwa majina yao, walidai kuwa
inashangaza kuona idara nyeti kama ya usalama wa taifa na jeshi la
polisi watendaji wake wanatajwa kuhusika katika matukio hayo ya utesaji
raia lakini hawakamatwi kuhojiwa na kuchukuliwa hatua.
Walisema kuwa badala yake umegeuzwa kuwa mchezo wa kufifisha na
kuwahamisha watu kwenye hoja hizo kwa kuibua matukio mengine ambayo
yanavaliwa njuga kwa nguvu nyingi pasipo sababu.
Afisa mmoja mstaaafu alitolea mfano suala la kutekwa, kuteswa kwa Dk.
Ulimboka akisema kuwa alishangazwa na kauli ya Inspekta Jenerali wa
Polisi, Said Mwema, kudai kwamba suala hi siri ya taifa.
“Ninashindwa kuelewa kwa nini polisi au vyombo vyovyote vya usalama
havijamkamata wala kumhoji ofisa wa Ikulu, Ramadhan Ighondu, aliyetajwa
kuhusika na tukio la Dk. Ulimboka,” alisema.
Aliongeza kuwa alichokisema akiwa mahututi hakitofautiani na
alichokisema baada ya kupona, lakini akahoji kwa nini polisi hawakuwahi
kumhoji Ighondu badala yake serikali ilikimbilia kulifungia gazeti la
MwanaHalisi lililoripoti taarifa hiyo.
“Huu ni mkakati wa makusudi wa kutopeleleza kitu kinachojulikana,
kwani wenye jukumu hili wanawajua watesaji au wanajua sakata lote nyuma
ya hili suala ndiyo maana hawapelelezi,” alisema.
Ofisa mwingine alidai kuwa matukio hayo likiwemo la Kibanda na mengine yanatoa tafsiri kuwa serikali haiwajibiki.
Alisema watu waache kusingizia kuwa nchi imeharibika, bali inaharibiwa na serikali kwa kutowajibika.
Alisema upelelezi matukio ya Ulimboka, Mwangosi na Kibanda unazidi
kusuasua huku vyombo hivyo vikiwa vimeibua suala jipya la video ya
Wilfred Lwakatare na kuhamisha mjadala wa wananchi.
“Tukio la Mwangosi picha zinaonyesha wazi alivyouawa, lakini pamoja na
wale waliomuua kuonekana, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa, na ninyi
waandishi mmeacha kuandika, hivyo hivyo suala la Kibanda limenyamaziwa
sasa, mnajihusisha na Lwakatare,” alisema ofisa huyo.
Usiku wa kuamkia Juni 27, 2012, watu wasiojulikana walimteka kisha kumpiga na kumjeruhi vibaya Dk. Ulimboka.
Pamoja na polisi kudai kuunda kamati ya uchunguzi, baadaye walitupiana
mpira wakidai hakuna kamati kama hiyo huku Ulimboka mwenyewe kutowahi
kuhojiwa hadi leo.
Kibanda naye alitekwa na kuteswa Machi 6, mwaka huu, lakini hadi leo
hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo wakati video ya
Lwakatare iliyoonekana mtandaoni Machi 11, polisi wamekwishachunguza na
kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani.
Akizungumzia uharaka huo wa kumkamata kiongozi huyo wa CHADEMA, ofisa
maarufu mstaafu wa idara ya usalama wa taifa alidai kuwa suala hilo
linapoteza heshima ya serikali kwani sasa inaonekana kulinda wauaji
wanaoua wanaharakati au watetezi wengine.
HABARI NA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment