SHULE ya Msingi Machala iliyopo Kata ya Miono, wilayani
Bagamoyo, Pwani, inakabiliwa na ukosefu wa vyumba vya madarasa, hali
inayosababisha wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba kusomea katika
chumba kimoja.
Pamoja na tatizo hilo, shule hiyo yenye wanafunzi 155, inahudumiwa na mwalimu mmoja tangu ilipoanzishwa miaka saba iliyopita.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Christopher Lutuku, anatumia chumba cha
stoo kama ofisi yake ya kuhifadhia vitabu na nyaraka mbalimbali za
kiofisi.
Hayo yalibainika juzi mjini Miono katika kikao cha Halmashauri Kuu ya
kata hiyo kilichoandaliwa na Mbunge wa Chalinze, Said Bwanamdogo, kwa
ajili ya kusikiliza kero mbalimbali za wakazi wa kata hiyo pamoja na
kuelezea yale aliyoyafanya katika kipindi cha miaka miwili na nusu tangu
achaguliwe.
Akitoa changamoto hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mihuga, Omari Nguya,
alisema shule hiyo tangu ianzishwe miaka saba iliyopita inahudumiwa na
mwalimu mmoja na kuongeza kuwa mwalimu mwingine aliyepangiwa katika
shule hiyo hivi karibuni hayupo.
Kutokana na hali hiyo, alimuomba mbunge huyo kuharakisha kushughulikia
tatizo hilo ili waweze kuletewa walimu wengine na kupata fedha za
ujenzi wa madarasa.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Lutuku alisema kwa mara
ya kwanza mwaka huu shule hiyo inatarajia kutoa wanafunzi wanaohitimu
darasa la saba, lakini matumaini ya kufaulisha ni madogo, kwani baadhi
ya vitabu vya darasa la saba hakuna na hata madarasa mengine wanatumia
kitabu kimoja kimoja kwa baadhi ya masomo na vya masomo mengine hakuna
kibisa.
Bwanamdogo aliahidi kushughulikia suala hilo haraka kuanzia ngazi ya
Ofisa Elimu wa Wilaya, ili shule hiyo iweze kupata walimu, vitabu na
fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na ofisi ya mwalimu.
No comments:
Post a Comment